DAR ES SALAAM, Juni 18, 2026 – Katibu Msaidizi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum, Bi. Elizabeth Komba, amewataka viongozi nchini kuwa mfano wa maadili mema kwa maneno, matendo na mwenendo wao wa kila siku ili kuimarisha utawala bora na kujenga imani ya wananchi kwa taasisi za umma.
Bi. Komba alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi yaliyofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Ushindani jijini Dar es Salaam tarehe 18 Juni 2026.
Alisema Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inaendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi na viongozi katika kusimamia na kukuza maadili ili kuimarisha uwajibikaji na utoaji bora wa huduma katika sekta ya umma.
“Viongozi wanapaswa kuwa kioo cha jamii kwa kuzingatia maadili katika maneno na matendo yao. Kwa kufanya hivyo, wataweza kusimamia maadili katika taasisi wanazoziongoza na kuhamasisha watumishi wengine kufuata misingi hiyo,” alisema Bi. Komba.
Aidha, alibainisha kuwa maadili na uadilifu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote duniani, kwani humjengea kiongozi heshima, uaminifu na kuthaminiwa na wananchi anaowahudumia.
Alisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kutenda haki kwa wote bila ubaguzi, upendeleo au misingi yoyote inayoweza kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.
Bi. Komba alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea viongozi uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, hatua itakayosaidia kuimarisha utoaji wa huduma za umma na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za Serikali.
Aliongeza kuwa viongozi wenye maadili na uadilifu ni msingi wa maendeleo endelevu, huku akiwataka washiriki wa mafunzo hayo kuyatumia maarifa waliyopata kuboresha utendaji kazi katika maeneo yao ya kazi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma za kuendelea kuimarisha misingi ya maadili, uwajibikaji na uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma nchini.


No comments:
Post a Comment