HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, June 7, 2026

DKT. MUYUNGI ATOA MWELEKEO WA BIASHARA YA KABONI

 


Na Mwandishi Wetu, Kagera
KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema kuwa maendeleo na ukuaji wa biashara ya kaboni nchini yanapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazochochea ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa wananchi katika kipindi cha miongo ijayo.

Dkt. Muyungi alitoa kauli hiyo leo mkoani Kagera wakati alipokutana na wadau wa biashara ya kaboni katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera. Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wataalamu wa mazingira, wadau wa sekta binafsi pamoja na wawakilishi wa taasisi zinazojihusisha na biashara ya kaboni.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Muyungi alisema Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha kuwa biashara ya kaboni inasimamiwa kwa ufanisi ili iweze kutoa manufaa ya kiuchumi kwa wananchi huku ikiendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Alieleza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaotarajiwa kuanza Julai 1, 2026 unatoa nafasi kubwa kwa sekta mbalimbali, ikiwemo biashara ya kaboni, kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

Alisema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili, hususan misitu, ambayo inaweza kutumika kuzalisha mikopo ya kaboni (carbon credits) na hivyo kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Aidha, alibainisha kuwa biashara ya kaboni imeendelea kuwa moja ya fursa mpya za kiuchumi duniani kutokana na kuongezeka kwa jitihada za kimataifa za kupunguza uzalishaji wa gesi joto zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.

“Serikali inaendelea kuweka mazingira bora yatakayowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika biashara ya kaboni ili waweze kunufaika na fursa zinazotokana na sekta hii. Tunahitaji kuhakikisha kuwa ukuaji wa sekta hii unaendana na malengo ya maendeleo ya taifa na matarajio yaliyowekwa katika Dira ya 2050,” alisema Dkt. Muyungi.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kuhakikisha kuwa biashara ya kaboni inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii zinazoshiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira. Aliongeza kuwa elimu kwa umma kuhusu fursa za biashara ya kaboni ni muhimu ili wananchi waweze kuelewa thamani ya rasilimali walizonazo na namna ya kuzitumia kwa maendeleo endelevu.

Aidha, aliwataka wadau wa biashara ya kaboni kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali ili kuhakikisha kuwa shughuli zote zinazofanyika zinakuwa na uwazi, uwajibikaji na manufaa kwa pande zote zinazohusika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa KADERES, Bw. Leonard Kachebonao, alisema kuwa taasisi hiyo imeendelea kupanua ushiriki wa wananchi katika biashara ya kaboni kupitia usajili wa wakulima wadogo na utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kiuchumi.

Alisema kuwa licha ya kampuni hiyo kuwa changa, tayari imefanikiwa kusajili wakulima wadogo wapatao 180,000 katika Mkoa wa Kagera, huku zoezi la usajili likiendelea katika wilaya mbalimbali za mkoa huo. Alieleza kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kutokana na uelewa unaozidi kuongezeka kuhusu fursa zinazotokana na biashara ya kaboni.

“KADERES imeendelea kufanya kazi kwa karibu na jamii ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika miradi ya kaboni. Hadi sasa tumefanikiwa kusajili wakulima 180,000 na bado tunaendelea na zoezi hilo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera,” alisema Bw. Kachebonao.

Alifafanua kuwa kwa sasa shughuli za kampuni hiyo zinafanyika katika karibu wilaya zote za Mkoa wa Kagera isipokuwa Manispaa ya Bukoba, ambapo maandalizi ya kuanza utekelezaji wa shughuli hizo yanaendelea. Aliongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata nafasi ya kushiriki na kunufaika na biashara ya kaboni.

Mbali na Mkoa wa Kagera, Bw. Kachebonao alisema KADERES imejipanga kupanua shughuli zake katika maeneo mengine ya nchi, ikiwemo mikoa ya Morogoro na Pwani, ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika miradi ya uhifadhi wa mazingira inayozalisha mikopo ya kaboni.

Alisema kuwa upanuzi huo utasaidia kuongeza mchango wa biashara ya kaboni katika maendeleo ya kiuchumi ya wananchi na taifa kwa ujumla, huku ukiimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali na wadau mbalimbali za kuendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika biashara ya kaboni, ambayo imeendelea kupata umuhimu mkubwa duniani kama moja ya suluhisho la kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad