Dar es Salaam, Julai 2026
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Ernest Mabonesho, ametangaza kuwa kilele cha maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo kitafanyika tarehe 3 Julai 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, kuanzia saa 3:00 asubuhi.Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Dkt. Mabonesho amesema kuwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kilianzishwa mwaka 2000 kwa lengo la kuimarisha utendaji, ufanisi na weledi katika utumishi wa umma nchini, na kwamba mwezi Agosti 2025 Chuo kilitimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.
Katika kuadhimisha miaka 25 ya Chuo, shughuli mbalimbali za kijamii, kitaaluma na maendeleo ya jamii zimetekelezwa katika kampasi zote sita za Chuo zilizopo Dar es Salaam, Tabora, Mtwara, Singida, Tanga na Mbeya.
Miongoni mwa shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na Utumishi Marathon 2025 iliyofanyika mkoani Mtwara, Mdahalo wa Kitaifa kuhusu matumizi ya Akili Unde (AI) katika Sekta ya Umma, pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Tanga uliofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb.), tarehe 20 Februari 2026.
Aidha, Chuo kupitia kampasi zake kimefanya shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii, ikiwemo kutoa misaada katika vituo vya kulelea wazee, watoto yatima, watoto wenye mahitaji maalum, vituo vya afya na magereza, pamoja na kutoa elimu ya maadili na uzalendo kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Pia, kwa kushirikiana na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar, Chuo kiliandaa Kongamano la Pili la Kitaaluma la Utumishi wa Umma Tanzania lililojadili nafasi ya utumishi wa umma katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumzia maadhimisho hayo, Dkt. Mabonesho amesema:
"Maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ni fursa muhimu ya kutathmini safari yetu, kuonesha mafanikio tuliyoyapata, kutambua mchango wa wadau wetu, na kuweka mwelekeo wa Chuo katika kuendelea kuimarisha utumishi wa umma wenye weledi, maadili na ufanisi nchini."
Dkt. Mabonesho ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 25, Chuo kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kupanua huduma zake kutoka kampasi mbili hadi kampasi sita, kuongeza programu za mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa mafunzo, pamoja na kuendeleza miundombinu na rasilimali watu.
Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kinawakaribisha wadau wote wa Chuo, wahitimu, watumishi wa umma, taasisi mbalimbali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wananchi kwa ujumla kushiriki katika tukio hili muhimu la kihistoria

No comments:
Post a Comment