Farida Mangube Morogoro
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu wawili, Bashiri Abdallah Matenga (22), dereva bodaboda mkazi wa mtaa wa Bomba la Zambia, kata ya Kingolwira Manispaa ya Morogoro, pamoja na Gabriel Daniel Issaya (26), dereva bodaboda mkazi wa Mkambarani wilayani Morogoro, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Brian Emanuel Mkilya (22), mkazi wa Mkoa wa Mara aliyekuwa akiishi kata ya Mkambarani wilayani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi hilo, imesema tukio hilo lilitokea Mei 17, 2026 majira ya saa 5 asubuhi katika eneo la Kingolwira, Manispaa ya Morogoro. Inadaiwa kuwa marehemu alishambuliwa na kundi la watu waliokuwa wamejichukulia sheria mkononi wakimtuhumu kuiba pikipiki.
Watuhumiwa ambao wote ni madereva bodaboda na wakazi wa Morogoro, wanaendelea kuhojiwa huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea ambapo Polisi wamesema hatua za kisheria zitachukuliwa mara baada ya upelelezi kukamilika.
Katika taarifa yake, Jeshi la Polisi limeonya wananchi dhidi ya tabia ya kujichukulia sheria mkononi, likieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha na kujeruhi watu wasiokuwa na hatia.
Aidha, wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapohisi kuwepo kwa vitendo vya uhalifu ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.


No comments:
Post a Comment