Vituo vya kutolea huduma za afya vimetakiwa kuboresha maoteo ya uagizaji wa dawa na kuzingatia mwenendo wa magonjwa katika maeneo yao ili kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana wakati wote na kuondokana na changamoto ya wananchi kukosa bidhaa hizo wanapohitaji huduma.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Thomas Rutachunzibwa, leo Mei 15, 2026 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha wateja na wadau wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma inayohudumia Mikoa ya Dodoma, Singida pamoja na Halmashauri ya Kiteto ya Mkoa wa Manyara.
“MSD inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha bidhaa muhimu za afya zinapatikana, zinatunzwa na kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Ni muhimu kwa vituo vya afya kufanya maoteo sahihi ya mahitaji yao ili kuondoa malalamiko ya wananchi kuhusu ukosefu wa dawa,” amesema Dkt. Rutachunzibwa.
Amesema serikali inaendelea kuweka kipaumbele kuhakikisha nidhaa za afya ziinapatikana wakati wote ili wananchi waendelee kupata huduma bora za afya.
Dkt. Rutachunzibwa amewataka watendaji wa sekta ya afya Halmashuari za Wilaya kushirikiana na wafamasia pamoja na wataalam wa maabara kupanga mahitaji ya dawa na kuhakikisha bidhaa hizo zinatengewa bajeti pamoja na kuwepo fedha za manunuzi.
“Kwa nini tuwe na dawa zinaharibika kutokana na kuagiza bidhaa nyingi kuliko mahitaji halisi wakati bado kuna wananchi wanahitaji huduma hizo? Ni muhimu kuboresha maoteo na kuagiza dawa kulingana na mwenendo wa magonjwa katika maeneo husika,” amesisitiza.
“Asitokee mtu mmoja anatengeneza oda na kuleta dawa ambazo hazihitajiki na kufanya tuwe na dawa zinazokwenda kuharibika bila matumizi,” amesema Dkt. Rutachunzibwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD, Hassan Ibrahim, amesema ushirikiano na mawasiliano ya karibu kati ya wadau wa sekta ya afya ni muhimu katika kuhakikisha changamoto za mnyororo wa ugavi zinatatuliwa kwa wakati.
“Tunatamani tuwe tunaongea lugha moja katika kutatua changamoto za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” amesema Hassan.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, amesema jukumu kubwa la MSD ni kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana kwa wakati kwa wateja wake kupitia ushirikiano wa karibu na wadau wa mnyororo wa ugavi.
Amesema vikao hivyo vinasaidia kupata mrejesho kutoka kwa wateja na kujadili namna bora ya kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya.

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)




.jpeg)



.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment