HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 1, 2026

TPSC DAR ES SALAAM KATIKA MAADHIMISHO YA MEI MOSI DAR ES SALAAM, Mei 1, 2026

Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam, leo wameungana na watumishi wengine wa taasisi za umma na binafsi kusherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani, maarufu kama Mei Mosi. Maadhimisho haya yamefanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, yakilenga kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika kuleta maendeleo ya taifa.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila, ambaye katika hotuba yake amewakumbusha wafanyakazi umuhimu wa kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii. Bw. Chalamila amesema, “Tunaposherehekea siku hii, ni muhimu kutambua kwamba wafanyakazi ndio wanaobeba taswira ya serikali. Mfanyakazi mmoja anaweza kusababisha serikali ichukiwe au ipendwe, hivyo kila mmoja wetu awajibike kwa ufanisi na uaminifu.”


Aidha, Bw. Chalamila amesisitiza kuwa serikali inawathamini na kuwapenda wafanyakazi wake, na anaamini kupitia juhudi zao, taifa litaendelea kupata mafanikio. Amewahimiza wafanyakazi wote kuendelea kujituma na kufanya kazi kwa moyo, kwa manufaa ya chuo, jamii na nchi kwa ujumla.


Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo: “Kazi zenye Staha ni Nguzo ya Kwanza kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” yakilenga kuhamasisha wafanyakazi kutoa mchango wao katika kujenga taifa kwa kuzingatia staha na haki mahali pa kazi.


Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi, pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, ambapo ujumbe mkuu umetolewa wa kuendelea kuthamini mchango wa wafanyakazi katika ustawi wa taifa.


Baada ya maadhimisho ya kimkoa, hafla maalum iliendelea katika Ukumbi wa Kilimanjaro uliopo katika Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao, ambapo Mkurugenzi wa Kampasi ya Dar es Salaam, Bw. Mussa Lugembe, alimwakilisha Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu katika hafla kwa kutoa hotuba fupi na kutoa zawadi kwa wafanyakazi hodari wa Kampasi ya Dar es Salaam na Makao Makuu, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuhamasisha utendaji bora kazini.


Akizungumza na watumishi kwa niaba ya Mkuu wa Chuo, Bw. Lugembe amewataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano ili kuhakikisha mafanikio ya chuo na taifa kwa ujumla. Amesisitiza kuwa watumishi wa umma, wanawajibika kusaidia serikali kutimiza malengo yake ya kuhudumia wananchi, huku wakizingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma.


“Tuendelee kuchapa kazi kwa maendeleo ya chuo chetu na tukumbuke kuwa sisi ni Watumishi wa Umma, wenye jukumu la kutimiza malengo ya serikali. Tufuate sheria, tujiepushe na migongano, na tuwe na mshikamano katika kazi,” alisema Bw. Lugembe.


Aidha, alisisitiza kuwa menejimenti ya chuo itaendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha wafanyakazi wanapata stahiki zao. Pia, alihimiza umuhimu wa kupenda taasisi na kuvumiliana ili kujenga umoja na mshikamano katika kutoa matokeo bora zaidi.


Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kushiriki maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ 2026 yaliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Grounds, jijini Dar es Salaam.



Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakiwa katika ushiriki wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ 2026 yaliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Grounds, jijini Dar es Salaam.


Bw. Mussa Lugembe, Mkurugenzi wa Kampasi ya Dar es Salaam, akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa niaba ya Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu. Picha zote na Emmanuel Massaka, Michuzi Tv.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad