.jpeg)
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, leo ameshiriki ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Ngurdoto, mkoani Arusha.
Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, na umewakutanisha zaidi ya wanachama 5,050 wa TAPSEA kutoka Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, taasisi mbalimbali za umma pamoja na wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi aliwataka wajumbe wa mkutano huo, ambao pia unatarajiwa kuchagua viongozi wapya wa chama hicho, kuzingatia haki, mshikamano na maslahi ya taasisi yao, huku akisisitiza umuhimu wa kuepuka migogoro na mambo yanayoweza kukipotezea mwelekeo chama hicho muhimu kwa maendeleo ya utumishi wa umma nchini.
Kwa upande wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete, akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, aliwakumbusha wajumbe hao juu ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha ustawi wa watumishi wa umma nchini.
Alieleza kuwa Serikali imeendelea kupandisha madaraja watumishi, kuboresha miundo na vyeo vya kazi, pamoja na kulipa madeni mbalimbali ya mishahara na stahiki za watumishi, huku akiahidi kuwa juhudi hizo zitaendelea kadri hali ya bajeti ya Serikali itakavyoruhusu.
“Tumekuwa tukifanya maboresho haya hatua kwa hatua, na dhamira yetu ni kuhakikisha watumishi wa umma wanaendelea kunufaika na matunda ya Serikali yao,” alisema Mhe. Ridhiwani.
Mkutano huo wa TAPSEA unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taaluma ya uandishi na uendesha ofisi pamoja na mustakabali wa chama hicho nchini.

.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment