HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 16, 2026

Tanzania mwenyeji wa Mkutano wa Uwekezaji

 

Mkurugenzi Mkuu wa ESRF Profesa Fortunata Makene akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Makutano wa kufungua fursa za uwekezaji utaofanyika mwezi ujao Mjini Arusha.
Mwakilishi Mkazi wa UNDP Shogeki Komatsubara akizungumza kuhusiana nafasi ya UNDP katika ushiriki wa mkutano wa kufungua fursa za uwekezaji katika mkutano utaofanyika Mjini Arusha Juni Mwaka huu.
Baadhi washiriki katika mkutano huo

*Miradi 60 ya Kimkakati Kuwasilishwa Kongamano la Uwekezaji Tanzania

Na Mwandishi Wetu
TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa Makutano wa Uwekezaji unaolenga kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.85 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi ESRF Profesa Fortunata Makene alisema kongamano hilo litafanyika Juni 1 hadi 2, 2026 katika Gran Meliá Arusha mkoani Arusha na Mgeni rasmi Waziri wa Mpingo na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo

Profesa Makene alisema mkutano huo utaunganisha wawekezaji wa kimataifa, taasisi za fedha, wadau wa maendeleo pamoja na waendelezaji wa miradi ya uwekezaji ya serikali iliyokamilisha maandalizi kwa ajili ya kupata mitaji.

Mkutano huo umeratibiwa Kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) ,Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania (TISEZA) pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar I(ZIPA).

Aidha, usajili kwa washiriki wa mkutano huo umefunguliwa rasmi ambapo wamiliki wa miradi ya umma, wawekezaji, waendelezaji wa miradi pamoja na taasisi za fedha za maendeleo wametakiwa kujisajili kupitia mfumo rasmi wa TIGF.

Profesa Makene alisema kongamano hilo litawakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za fedha, mifuko ya hifadhi ya jamii, wawekezaji binafsi pamoja na taasisi za kifedha kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema lengo kuu ni kuhakikisha mazungumzo ya uwekezaji yanazaa matokeo halisi kupitia miradi 60 iliyopitiwa na kuthibitishwa yenye thamani ya takribani dola bilioni 2.85 za Marekani.

Miradi hiyo inahusisha sekta mbalimbali za kipaumbele ikiwemo utalii na miundombinu ya asili, nishati jadidifu, usafirishaji, uchumi wa buluu Zanzibar, usindikaji wa mazao, miundombinu ya maji pamoja na miradi ya maendeleo ya ngazi za chini.

Waandaji wa kongamano hilo pia wametangaza kuwepo kwa miradi kati ya nane hadi 10 yenye kipaumbele kikubwa inayotarajiwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 100 za Marekani kila mmoja.

Profesa Makene alisema Tanzania ipo tayari kubadilisha fursa zilizopo kuwa miradi yenye tija ya kibiashara kwa manufaa ya taifa.

“TIGF 2026 ndiyo jukwaa ambalo jumuiya ya wawekezaji wa kimataifa itaweza kupata fursa hizi na kufuatilia kila hatua ya uwekezaji hadi pale makubaliano yatakapokamilika,” alisema Profesa Makene.

Amesema Tanzania inatarajia kunufaika zaidi na uwekezaji endelevu kupitia mkutano huo unaolenga kuharakisha mtiririko wa uwekezaji nchini na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uwekezaji barani Afrika.

Aidha, alisema kongamano hilo litakuwa daraja muhimu kati ya vipaumbele vya maendeleo ya taifa na mtaji wa kimataifa unaohitajika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Mataifa Nchini Tanzania (UNDP) Shigeki Komatsubara alisema taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kukuza maendeleo yanayoendeshwa na uwekezaji.

“UNDP Tanzania ipo tayari kusaidia Tanzania kuwezesha jukwaa linalokidhi viwango vya wawekezaji wa kimataifa,” alisema Komatsubara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad