Dar es Salaam- Mei 5, 2026: Mkurugenzi Mkuu wa Shule ya Serikali Kenya (KSG), Prof. Nura Mohamed na ujumbe wake wametembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania leo, Mei 5, 2026, jijini Dar es Salaam.
Katika kikao cha pamoja na Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, chini ya Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho, wamejadiliana kwa kina kuhusu mikakati ya kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo, huku lengo likiwa ni kuboresha utendaji wa utumishi wa umma kwa kuwajengea uwezo watumishi na Tafiti Tumizi.
Aidha, alisisitiza kuwa, kutokana na uzoefu wa zaidi ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa KSG, ni fursa adhimu kwa TPSC kujifunza na kupata uzoefu wa kuboresha utumishi wa umma nchini Tanzania, ili kujenga utumishi wa umma imara.
Dkt. Mabonesho ameongeza kuwa, mashirikiano pia yanalenga kujenga utumishi wa umma wenye tija, wenye kuzingatia matokeo, na kuleta maendeleo chanya kwa wananchi wa Tanzania, Kenya, na jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Prof. Mohamed amesisitiza kuwa, ushirikiano huo utahusisha pia kufanya tafiti za pamoja kuhusu kuboresha sera na huduma zinazohudumia jamii, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, ambazo ni haki yao ya msingi.
Ziara hiyo pia iliwapa nafasi ujumbe kutoka KSG kutembelea Makao Makuu ya Chuo yaliyopo Barabara ya Bibi Titi, Kampasi ya Dar es Salaam iliyopo Magogoni, na Kituo cha Mafunzo kwa njia ya Mtandao, ambapo walijionea mazingira ya mafunzo na shughuli zinazofanywa na chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.

No comments:
Post a Comment