HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 12, 2026

Shule ya Sekondari ya WAJA BOYS Yaongoza Kitaifa Hisabati (Basic Mathematics) - 2025

Shule ya Sekondari ya WAJA BOYS imeibuka kinara wa matokeo ya kitaifa ya Kidato cha Nne mwaka 2025 katika somo la Hisabati (Basic Mathematics), mafanikio ambayo yameelezwa kuwa ni matokeo ya dira na mikakati ya muda mrefu ya shule hiyo katika kuinua kiwango cha elimu nchini.


Uongozi wa shule hiyo umeeleza kuwa kwa zaidi ya miaka 10, WAJA BOYS imekuwa ikitekeleza dira ya kuwa miongoni mwa shule bora nchini katika utoaji wa elimu yenye ushindani mkubwa, hasa katika masomo ya Sayansi na Hisabati ambayo yana mchango mkubwa katika soko la ajira la sasa.

Mkuu wa shule hiyo, Shabo Shipembo, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu, hususan kuajiri walimu wenye taaluma, uzoefu na uwezo mkubwa wa kufundisha somo la hisabati.

“Hisabati ni miongoni mwa masomo yenye changamoto kwa wanafunzi wengi, hivyo tumeamua kuwekeza zaidi katika walimu bora na mbinu za kisasa za ufundishaji ili kuhakikisha wanafunzi wetu wanafanya vizuri,” amesema Shipembo.

Kwa upande wake, Kaka Mkuu wa shule hiyo, Musa Hamza, amesema shule imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kuweka mifumo inayowawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu na ufanisi mkubwa.


Naye mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika shule hiyo, Peniel Paulo, amesema mafanikio ya wanafunzi yanachangiwa na utaratibu wa kufanya tathmini za mara kwa mara pamoja na uwepo wa vipindi maalum vya hisabati vinavyoandaliwa kila wiki.


Amesema walimu waliopo shuleni hapo wana uwezo mkubwa wa kufundisha na kuwajengea wanafunzi uelewa wa kina katika somo la hisabati, jambo ambalo limeendelea kuongeza ufaulu wa shule hiyo mwaka hadi mwaka.

Mafanikio ya WAJA BOYS yanaendelea kuiweka shule hiyo katika nafasi ya juu kitaifa na kuwa mfano wa kuigwa katika maendeleo ya elimu ya Sayansi na Hisabati nchini Tanzania.

2 comments:

Post Bottom Ad