Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatayofanyika Juni 5 mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiwa na Wakuu wa Taasisi zilizo kuwa Chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais wakimsikiliza kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatayofanyika Juni 5 mwaka huu.
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema inatarajia kuzindua mpango mkakati maalum wa mazingira utakaotekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030 katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usimamizi wa mazingira nchini.
Hayo ameyasema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu was Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wakati akitangaza Siku ya Mazingira Duniani itayofanyika Juni 5 Mwaka huu.
Masauni, amesema mkakati utaozinduliwa unalenga kushughulikia kwa kina changamoto mbalimbali za kimazingira, ikiwemo taka ngumu mijini, matumizi yasiyo endelevu ya ardhi, uharibifu wa mazingira na usimamizi wa mifumo ya uzalishaji.
Amesema mpango huo utaelekezwa katika maeneo yote muhimu bila kuacha sekta yoyote nyuma, ukiwemo upandaji miti, usimamizi wa mifugo, udhibiti wa taka za plastiki pamoja na uimarishaji wa mifumo ya mazingira mijini na vijijini.
Waziri Masauni amebainisha kuwa Serikali pia imejipanga kuimarisha taasisi zinazosimamia mazingira ili ziwe na uwezo wa kutosha kiutendaji, wataalamu wenye weledi na rasilimali za kutosha katika kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unafanyika kwa ufanisi na kuwa endelevu
Amesema mageuzi yatayofanyika ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha nchi inakuwa na mfumo imara wa usimamizi wa mazingira unaoweza kukabiliana na changamoto zilizopo na zijazo.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inalenga kubadili taka kuwa fursa ya kiuchumi, ambapo taka zitachakatwa na kutumika kuzalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo nishati na bidhaa za viwandani, hatua itakayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza tija ya kiuchumi.
Amesema katika kuelekea maadhimisho hayo kutafanyika makongamano mbalimbali ikiwemo na elimu kwa wananchi ili kuweza kuwa na uelewa wa suala la mazingira.
Hata hivyo amesema moja ya kongomano litakalofanyika ni katika maadhimisho ya miaka 40 ya Baraza la Usimamizi na Uhifadhi Mazingira (NEMC).
Amesema katika jitihada zingine Serikali kuendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti ambapo kuelekea maadhimisho hayo watapanda Miti Wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Waziri Masauni amesema uzinduzi rasmi wa mpango huo unatarajiwa kufanyika katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira yatakayofanyika tarehe 5, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.





No comments:
Post a Comment