HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 29, 2026

MIAKA 18 BAADAYE: JK AKUTANA TENA NA CATHERINE, BINTI ALIYEFANYIWA UPASUAJI WA MOYO AKIWA NA MIAKA MINNE

 



RAIS  mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, leo Mei 29, 2026 amekutana tena na Bi. Catherine P. Conrad Minja, aliyefanyiwa upasuaji wa moyo kwa mafanikio akiwa na umri wa miaka minne katika taasisi ya Muhimbili Orthopaedic Institute (MOI) miaka 18 iliyopita.

Wakati huo madaktari bingwa wa Moyo wa JKCI walikuwa wakitumia majengo ya MOI kabla jengo lao halijakamilika.

Mara ya kwanza wawili hao walikutana Novemba 14, 2008 wakati Dkt. Kikwete akiwa Rais alipokwenda kumjulia hali Catherine hapo MOI baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo mapema wiki hiyo. Wakati huo Catherine alikuwa mmoja wa wagonjwa wa mwanzo kufanyiwa upasuaji huo katika taasisi hiyo.

Miaka 18 baadaye, Catherine amekua na sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Kairuki jijini Dar es salaam.

Alifika ofisini kwa Rais Mstaafu kumsabahi na kumshukuru kwa mchango wake katika kuanzisha na kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo nchini.

Dkt. Kikwete alimpongeza Catherine kwa kutimiza ndoto yake ya kusomea udaktari, jambo ambalo aliahidi kulifanya alipokuwa mtoto. Alisema amefurahishwa kumuona akiwa mwenye afya njema na akijiandaa kulitumikia taifa kupitia taaluma ya tiba.

Kwa upande wake, Catherine alisema anatamani kuwa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo ili kuwasaidia wagonjwa wenye changamoto kama aliyowahi kupitia yeye mwenyewe, akieleza kuwa hiyo itakuwa ni moja ya njia ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na afya njema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad