MONACO - Benki ya CRDB imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya Taifa kupitia sekta mbalimbali kwa kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 81 wa Michezo ya Majeshi Duniani (81st CISM General Assembly) uliofanyika nchini Monaco kuanzia tarehe 1 hadi 9 Mei 2026.
Mkutano huo wa kimataifa uliwakutanisha viongozi wa kijeshi na wadau wa michezo kutoka zaidi ya nchi 130 duniani kwa lengo la kuimarisha mshikamano, diplomasia ya michezo na amani kupitia kaulimbiu ya “Friendship Through Sport.”
Benki ya CRDB, ikiwa miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo nchini, imeendelea kuunga mkono jitihada za vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na michezo ya majeshi, hatua inayoimarisha ushirikiano wake na taasisi za Serikali katika kukuza ustawi wa askari na familia zao.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Brigedia Jenerali Saidi Hamisi Saidi, akisaidiana na Luteni Kanali Penina Anthony Igwe. Kutoka CRDB, ujumbe unajumuisha Meneja wa Kitengo cha Wateja Maalum, Crispin Sichalwe pamoja na Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Emmanuel Tupeligwe.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Sichalwe alisema CRDB imeendelea kutoa huduma maalum za kifedha kwa wanajeshi ndani na nje ya nchi, ikiwemo mikopo nafuu, bima na huduma za kifedha zinazowafikia popote walipo.
“Tunatambua mchango mkubwa wa majeshi katika usalama wa Taifa, hivyo tunahakikisha wanapata huduma bora na za haraka kupitia kitengo chetu maalum,” alisema.
Kwa upande wake, Tupeligwe alisisitiza kuwa CRDB itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia elimu ya fedha na huduma zinazowafikia wanajeshi hata wakiwa katika maeneo ya mbali au majukumu ya kimataifa.
Aidha, benki hiyo imeendelea kuimarisha ushirikiano wake wa kimkakati na JWTZ ili kuhakikisha wanajeshi wanapata huduma bora za kifedha kwa urahisi, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika maendeleo na usalama wa Taifa.






No comments:
Post a Comment