HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, April 19, 2026

WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WATENDAJI SERIKALINI

 


*Awataka wahakikishe miradi inasimamiwa na kuleta tija iliyokusudiwa

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema watendaji wa Serikali wanajukumu la kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotokelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ya maji, umeme, afya, miundombinu na elimu inasimamiwa ipasavyo ili Watanzania waweze kupata tija iliyokusudiwa.

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka jitihada kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo ni lazima itekelezwe kama ilivyokusudiwa.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Aprili 19, 2026) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Msanga, Chamwino mkoani Dodoma baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa maji akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema jukumu kubwa walilonalo watendaji ni kusimamia ipasavyo miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na kuhakikisha wananchi wananufaika kama ilivyokusudiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na rasilimali za Taifa kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao. “…Watanzania waweze kunufaika na matunda ya Taifa lao.”

Pia, Waziri Mkuu amewaasa Watanzania kujiepusha na watu wanaotumia kivuli cha imani za dini kufanya siasa za majukwaani, huku wakiwa na lengo ovu la kuwagawa watanzania kwa chuki za kiiimani na itikadi za kisiasa. “Ndugu zangu Watanzani tuendelee kulinda umoja na amani yetu. Kuna watu sasa wanatafuta namna ya kutumia siasa na dini ili kutugawa, tujihadhari na watu wa namna hiyo” amesisitiza.

Awali,Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la mradi wa Maji wa Miji 28 wilayani Chamwino, ambapo alitumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa mradi huo akisema ni wa kimkakati unaokwenda kumaliza tatizo la maji katika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema Wizara ya Maji itahakikisha mradi huo mkubwa unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika. “Kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha nyingi na tayari vijiji 10,758 vimeshafikiwa na huduma ya maji safi na salama na vimebakia vijiji 1,575.”

Akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji Mijini kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Charles Mafie alisema kwamba mkataba wa mradi huo unatarajiwa kukamilika Agosti 10, 2026 ukiwa na thamani ya shilingi Bilioni 17.2 na umefikia asilimia 70.2 ya utekelezaji.

Mradi huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 60,000 katika kata za Msanga, Buigiri, Chamwino na Mtumba na kuongeza upatikanaji wa maji safi kutoka asilimia 91 hadi 100 pamoja na kuimarisha uzalishaji wa maji kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadae.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad