HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 18, 2026

WAHANGA WA MAFURIKO KILOSA NA MVOMERO WAGUSWA NA KANISA.

 Na Maiko Luoga  - Morogoro 

Wahanga elfu moja na miatano wa majanga ya mafuriko kutoka kaya mia tatu za wilaya ya Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro, wamepewa msaada wa mahitaji ya kibinadamu ili kujikimu na maisha.

Msaada huo umetolewa na Shirika la kidini Norwegian Church AID kutoka nchini Norway, kwa kushirikiana na Kanisa Anglikana Dayosisi ya Morogoro, kupitia shirika la maendeleo (Devotional and Dedicated Services Community Development Organisation, (DDSCDO).

Akizungumza wakati wa kutoa mahitaji hayo 17 aprili 2026, Askofu Godfrey Sehaba wa Dayosisi ya Morogoro, Kanisa Anglikana Tanzania alisema, Dayosisi na shirika la Norwegian Church AID wametoa vifaa hivyo ili kuwa sehemu ya faraja kwa wahanga.

"Kanisa lina wajibu wa kugusa maisha ya watu kupitia shida zao, Kristo ametuagiza kupendana sisi kwanza ili tuweze kumwona Mungu" alisema Askofu Sehaba.

Zoezi la kugawa misaada hiyo lilifanyika katika Kijiji cha Tindiga, wilayani Kilosa na kuhudhuriwa na wawakikishi wa serikali Bi. Salome Mkinga, Afisa Tawala wilaya ya Kilosa na Bi. Mary Kayowa, Mkuu wa Divisheni ya Maliasili na Hifadhi ya mazingira wilaya ya Mvomero.

Theonat Mushi, kutoka Norwegian Church Aid alisema, Shirika limeguswa na majanga hayo yaliyowafika wananchi wa wilaya za Kilosa na Mvomero, na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Dayosisi ya Morogoro na serikali katika kusaidia wahanga hao.

"Tunatambua mafuriko haya yameleta changamoto kubwa katika familia zenu, mmekosa mahali pa kuishi na kupoteza mali, Tumefika hapa kutoa sehemu ya msaada wa mahitaji ili kuwapa faraja" alisema Theonat Mushi.

Bw. Kassimu Pazzi na Bi, Mellesiana Maganga, wahanga wa majanga ya mafuriko ya tarehe 17 hadi 18 Disemba 2025 katika Kijiji cha Tindiga, wameshukuru Kanisa Anglikana Dayosisi ya Morogoro kwa kufika na kutoa mkono wa faraja kwao.

"Tunaushukuru uongozi wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Morogoro kwa kuja kutoa msaada wa mahitaji kwetu, tunaoishi katika Kambi hapa Tindiga, Mungu awabariki sana" walisema wahanga wa mafuriko - Tindiga - Kilosa.

Baadhi ya mahitaji yaliyotolewa ni pamoja na Magodoro, Mablanketi, Sabuni, vitakasa mikono, vifaa vya kutibu maji ya kunywa na mahitaji mengine muhimu ya binadamu.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad