
Mashindano ya mchezo wa chess kwa watoto, Tanzanite Junior Chess Championship, yamefanyika jijini Dar es Salaam, yakileta pamoja washiriki kutoka shule mbalimbali nchini katika tukio lililojaa ushindani mkali, furaha na kujifunza.
Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Tanzanite Legacy Chess Club, Bi. Hellen Ulaya, aliwashukuru wazazi na walezi kwa mchango wao mkubwa wa kuwahamasisha watoto kushiriki. Alisisitiza kuwa ushiriki wa wazazi ni msingi muhimu katika kukuza vipaji na maendeleo ya watoto.
Bi. Ulaya alieleza kuwa mchezo wa chess ni nyenzo muhimu katika kukuza uwezo wa watoto kufikiri kwa kina, kufanya maamuzi sahihi pamoja na kujenga nidhamu na umakini, hali inayochangia pia mafanikio yao darasani na katika maisha ya kila siku.
Alifafanua kuwa lengo la mashindano hayo ni kuibua na kukuza vipaji vya watoto katika chess, kujenga kizazi chenye fikra makini na kuandaa mabingwa watakaoweza kulipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa. Aidha, mashindano hayo yanalenga kuhamasisha ujifunzaji kupitia michezo huku yakijenga urafiki, ushirikiano na ushindani wa afya miongoni mwa watoto.
Kwa upande wa haki za watoto, Bi Ulaya alisisitiza kuwa kila mtoto anapaswa kupata fursa ya kushiriki katika michezo ya maendeleo ya akili bila kujali hali ya kifedha, akitoa wito kwa wadau kushirikiana kueneza mchezo wa chess mashuleni na katika jamii.
Mashindano ya Tanzanite Junior Chess Championship yameendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa watoto wengi, yakitarajiwa kufanyika kila mwaka ili kutoa fursa kwa vipaji vipya kuibuka na kuimarika zaidi katika mchezo huo.







No comments:
Post a Comment