Serikali ya Tanzania imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuboresha makazi holela na kuyageuza kuwa maeneo rasmi, salama na yenye huduma bora, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na kasi kubwa ya ukuaji wa miji nchini.Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki jijini Nairobi nchini Kenya na Waziri wa Ardhi. Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo katika mjadala maalum uliofanyika pembezoni mwa Kongamano la Pili la Miji Afrika (2ND Afrika Urban Forum), ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili mbinu jumuishi za kuleta mageuzi katika makazi holela.
Amesema, Tanzania kama zilivyo nchi nyingi zinazoendelea, inashuhudia ongezeko kubwa la watu wanaohamia mijini, hali inayosababisha shinikizo katika upangaji wa miji, utoaji wa makazi, usimamizi wa ardhi pamoja na huduma za kijamii na kiuchumi.
Ameeleza kuwa, katika kipindi cha zaidi ya nusu karne, idadi ya watu wanaoishi mijini imeongezeka kwa kasi kutoka asilimia 5.7 mwaka 1967 hadi kufikia asilimia 34.9 mwaka 2022, huku makadirio yakionesha kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi hiyo itafikia asilimia 59.
‘’Ukuaji huu unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kasi ya ukuaji wa miji katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara’’. amesema
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ukuaji huo umeambatana na kuongezeka kwa makazi holela, ambapo takribani asilimia 67.3 ya makazi yote mijini yapo katika maeneo yasiyopangwa.
Kutokana na changamoto hiyo, Dkt Akwilapo ameeleza kuwa, Serikali ya Tanzania imechukua hatua za kimkakati zinazolenga kuboresha makazi hayo badala ya kuyabomoa, kwa kutumia mbinu za upangaji shirikishi, uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa huduma muhimu kama maji, barabara na umeme.
Amesema, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya Watu ya mwaka 2000 pamoja na Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 iliyoboreshwa mwaka 2023, zinaelekeza wazi kuwa makazi holela yataboreshwa na kurasimishwa ili kuhakikisha wakazi wanapata haki ya umiliki wa ardhi na huduma za msingi.
Aidha, ameweka wazi kuwa, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa urasimishaji wa makazi holela kwa kuwapatia wananchi hati miliki za ardhi, hatua inayochochea uwekezaji na kuwezesha wananchi kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.
‘’Mpango huo pia unalenga kubadilisha rasilimali zisizo rasmi kuwa mali zenye tija katika uchumi wa nchi’. amesema
Aidha, Dkt Akwilapo amesema, Serikali ya Tanzania pia imeanzisha programu maalum ya upangaji upya wa ardhi (land readjustment) inayolenga kuboresha maeneo chakavu yaliyopo katikati ya miji, ili kuyafanya yaweze kutumika kwa ufanisi zaidi kiuchumi na kijamii.
Akihitimisha wasilisho lake Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisisitiza kuwa makazi holela hayapaswi kuonekana kama tatizo pekee, bali kama sehemu ya fursa za kiuchumi na ubunifu kwa wananchi wengi.
Aalitoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana katika kuunganisha mipango rasmi ya miji na hali halisi ya makazi holela, ili kujenga miji himilivu, jumuishi na inayokidhi mahitaji ya wote bila kumuacha mtu nyuma, kwa kuzingatia malengo ya Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akiwasilisha taarifa ya hali ya urasimishaji makazi holela wakati wa mjadala maalum uliofanyika pembezoni mwa Kongamano la Pili la Miji Afrika (2ND Afrika Urban Forum), ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili mbinu jumuishi za kuleta mageuzi katika makazi holela.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akiwa na mawaziri wenzake kutoka Ghana Mhe. Kenneth Gilbert Adjei, Waziri wa Ujenzi, Nyumba na Rasilimali za Maji (kushoto) na Malawi Mhe. Chimwemwe Chipungu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji (wa pili kulia) wakifuatilia uwasilishwaji taarifa ya hali ya makazi holela kutoka kwa Mhe. Balla Moussa Fofana, Waziri wa Mipango Miji, Serikali za Mitaa na Maendeleo ya Maeneo Senegal wakati wa mjadala maalum uliofanyika pembezoni mwa Kongamano la Pili la Miji Afrika (2ND Afrika Urban Forum) jijini Nairobi nchini Kenya mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (wa pili kushoto) Mhe. Kenneth Gilbert Adjei, Waziri wa Ujenzi, Nyumba na Rasilimali za Maji kutoka Ghana (kushoto) na Mhe. Chimwemwe Chipungu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji Malawi (wa pili kulia) wakifuatilia uwasilishwaji taarifa ya hali ya makazi holela wakati wa mjadala maalum uliofanyika pembezoni mwa Kongamano la Pili la Miji Afrika (2ND Afrika Urban Forum) jijini Nairobi nchini Kenya mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akiwa na mawaziri wenzake kutoka nchi za Ghana, Malawi na Senegali wakati wa mjadala maalum uliofanyika pembezoni mwa Kongamano la Pili la Miji Afrika (2ND Afrika Urban Forum), ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili mbinu jumuishi za kuleta mageuzi katika makazi holela.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akichangia hoja wakati wa mijadala iliyofanyika pembezoni mwa Kongamano la Pili la Miji Afrika (2ND Afrika Urban Forum) jijini Nairobi nchini Kenya mwishoni mwa wiki.

Sehemu ya washiriki wa mijadala mbalimbali iliyofanyika pembezoni mwa Kongamano la Pili la Miji Afrika (2ND Afrika Urban Forum) jijini Nairobi nchini Kenya mwishoni mwa wiki. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)





No comments:
Post a Comment