HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 11, 2026

Tanzania Kuendeleza Uwiano kati ya Maendeleo ya Uchumi, Uendelevu wa Mazingira na Usalama wa Bahari

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema Tanzania inaendelea kujizatiti kusawazisha maendeleo ya kiuchumi, uendelevu wa mazingira, na usalama wa bahari.

Waziri Kombo amesema hayo alipozungumza katika Mkutano wa Tisa wa Bahari ya Hindi Aprili 10 2026, jijini Port Louis, Mauritius.

“Tanzania, kupitia juhudi za uhifadhi, ushirikishwaji wa jamii, na ushirikiano wa kikanda, inaendelea kulinda mifumo ya ikolojia ya bahari ya Hindi na kuimarisha usalama katika maji ya eneo lake, Ila mafanikio ya kudumu yatategemea ushirikiano imara zaidi kati ya nchi zinazopakana na bahari ya Hindi”, alisisitiza.

Balozi Kombo alihimiza nchi zinazopakana na bahari ya Hindi kuthibitisha wajibu wa pamoja na kushirikiana kuilinda bahari hiyo ili iendelee kuwa chanzo cha amani, ustawi, na fursa kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Alieleza kuwa Bahari ya Hindi ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi na ushirikiano wa kikanda kwa Tanzania, na ni lango muhimu linalounganisha nchi jirani zisizo na bandari na masoko ya dunia.

Aidha, alieleza kuwa kupitia uwekezaji wa kimkakati katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ya bandari na nishati, Tanzania inaendelea kujiweka kama kitovu muhimu cha biashara, usafirishaji na huduma za baharini katika Afrika Mashariki na Kati na kwamba uchumi wa buluu unachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa, ukisaidia mamilioni ya watu na kukuza sekta za uvuvi, utalii, usafiri wa baharini na biashara za pwani.

Balozi Kombo alisema kaulimbiu ya mkutano huo ya “Uwajibikaji wa Pamoja kwa Usimamizi wa Bahari ya Hindi,” inaendana kikamilifu na hali halisi kwa sasa, na kwamba Bahari ya Hindi inakabiliwa na changamoto za mvutano wa kisiasa, vitisho vya usalama wa baharini vinavyoendelea kubadilika, pamoja na shinikizo la kimazingira.

“Changamoto hizi zinaonyesha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa husika na kuwa uwajibikaji wa pamoja si hiari tena ni suala la lazima ili kuhakikisha kuwa bahari ya Hindi inakuwa salama, endelevu, na yenye manufaa kwa wote wanaoitegemea,” alisisitiza.













No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad