Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkubwa wa kitaifa utakaowakutanisha wauzaji chakula (Mamalishe na Babalishe) kutoka mikoa yote nchini.
Mkutano huo umepangwa kufanyika Aprili 11, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumamosi Aprili 4,2026 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Wauzaji Chakula nchini kupitia Umoja wa Mamalishe na Babalishe Tanzania (UMALITA), Avijawa Omari, amesema kuwa wanaiomba Serikali kuwatambua rasmi kama kundi muhimu katika uchumi wa nchi.
Amesema kuwa utambuzi huo utawawezesha wanachama kupata mikopo, fursa za kiuchumi na kukuza ajira kwa vijana na wanawake nchini.
“Tunaomba Serikali ituone rasmi. Utambuzi utarahisisha upatikanaji wa mikopo na kutupa nafasi ya kupanua biashara zetu ili tuzalishe ajira zaidi,” amesema.
Bi Omari ameongeza kuwa mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu kwa mamalishe na babalishe kuwasilisha moja kwa moja changamoto zao kwa viongozi wa Serikali kwa lengo la kuongeza kipato, kupanua biashara na kuchangia ukuaji wa ajira nchini.
Aidha, amewataka wanachama na wauzaji chakula wote nchini kujitokeza kwa wingi Aprili 11 katika ukumbi wa JNICC ili kujenga kwa pamoja mustakabali wa biashara zao.
Mkutano huo utafanyika chini ya kaulimbiu “Pika Kishua, Vaa Kishua” (Cook Smart, Dress Smart), inayolenga kuboresha viwango vya utoaji huduma na kuimarisha taswira ya kitaalamu ya wauzaji chakula nchini.
“Sisi ni wajasiriamali tunaojitegemea, na tunalisha taifa asubuhi, mchana, jioni hadi usiku. Tunaomba jamii itambue mchango wetu na kuheshimu kazi tunayoifanya,” aliongeza.
Ameeleza pia kuwa sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo hatari za kiafya na mazingira magumu ya kazi, lakini sasa wameanza kuelekea katika matumizi ya nishati safi na mbinu bora za upishi ili kulinda afya na kukuza biashara.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Babalishe, Ndugu Ngosha, amesisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano miongoni mwa wanachama ili kufikia malengo yao ya kiuchumi na kijamii.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa wa kihistoria kwa kuwaunganisha wadau wakuu wa sekta isiyo rasmi na viongozi wa juu wa Serikali kujadili mustakabali wa ajira na ujasiriamali nchini.






No comments:
Post a Comment