JESHI la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kufuatia taarifa iliyochapishwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii na Hilda Newton tarehe 10 Aprili 2026, ikidai kuwa Serikali imepanga kumuua Mbunge Tundu Lissu kwa risasi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, uchunguzi huo unalenga kubaini ukweli wa madai hayo pamoja na kukusanya ushahidi utakaosaidia hatua za kisheria kuchukuliwa.
Katika hatua ya kukamilisha uchunguzi huo, Jeshi la Polisi limemuelekeza Hilda Newton kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) iliyopo katika Jengo la Makao Makuu Ndogo ya Polisi, Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, tarehe 24 Aprili 2026 saa nne asubuhi.
Polisi wamesema kuwa lengo la kumuita ni kumpa fursa ya kuwasilisha ushahidi alioudai kuwa anao, ili kusaidia uchunguzi unaoendelea kufanyika kwa mujibu wa sheria.
Hatua hiyo inafanyika kwa mujibu wa kifungu cha 11(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, kinachoruhusu mamlaka husika kumuita mtu yeyote mwenye taarifa muhimu katika uchunguzi wa jinai.
Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kuepuka kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho ambazo zinaweza kusababisha taharuki au kuvuruga amani ya nchi.

.jpg)
No comments:
Post a Comment