HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 16, 2026

PICF 2026 KUIWEKA DAR KWENYE RAMANI YA VICHEKESHO DUNIANI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Jiji la Dar es Salaam linatarajia kuandika historia mpya katika tasnia ya burudani baada ya kutangazwa kwa uzinduzi wa tamasha la kwanza la kimataifa la vichekesho, Punchline International Comedy Festival (PICF) 2026, litakalofanyika kuanzia Mei 25 hadi Juni 1, 2026.

Tamasha hilo lililotangazwa na Punchline Africa, linatarajiwa kuwakutanisha wachekeshaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa kipindi cha wiki moja, likijumuisha maonesho ya jukwaani, shughuli za vyombo vya habari pamoja na ubadilishanaji wa utamaduni. Kilele cha tamasha hilo kitakuwa Grand Finale itakayofanyika katika ukumbi wa The Superdome.

PICF 2026 itahusisha maonesho ya vichekesho kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, hatua inayolenga kuonesha utofauti wa vipaji vya wacheshi barani Afrika. Waandaaji wamesema mbali na burudani, tamasha hilo lina lengo la kuhamasisha umuhimu wa vichekesho katika kuboresha afya ya akili kwa kuwapa watu nafasi ya kucheka, kupunguza msongo wa mawazo na kuunganishwa kijamii.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwanzilishi Mwenza wa Punchline Africa, Evans Bukuku, alisema tamasha hilo ni jukwaa muhimu la kuleta watu pamoja na kuwapa nafuu ya kihisia kupitia sanaa ya uchekeshaji.“Comedy siyo kuchekesha tu, ni njia ya kuelewa maisha na kupunguza msongo wa mawazo. Kupitia PICF tunataka watu waondoke wakiwa na nafuu hata kama changamoto bado zipo,” alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini, Anne Sophie Ave, alisema wameamua kuunga mkono tamasha hilo kutokana na mchango wa sanaa katika kukuza vipaji vya vijana na kuwajengea kujiamini.

Aliongeza kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na nafasi yake kama kitovu cha Afrika Mashariki na historia yake katika harakati za Pan-Afrika, akisisitiza kuwa sanaa ya vichekesho inaweza kuwa daraja la kuunganisha bara hilo.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu nchini, Emmanuel Ndumukwa, alisema serikali inaunga mkono juhudi hizo na kuona kuwa tamasha hilo linaweza kuwa chachu ya kukuza tasnia ya uchekeshaji nchini.

Kwa upande wa wasanii, mchekeshaji Humphrey Richard alisema PICF 2026 ni fursa adhimu kwa wacheshi kujifunza, kubadilishana uzoefu na kufikia masoko ya kimataifa.
Tamasha hilo linaandaliwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo Alliance Française Dar es Salaam, Tanzania Film Board pamoja na SGA Security.

Aidha, PICF ni sehemu ya mradi wa Création Africa unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa, unaolenga kuwawezesha wasanii na taasisi za ubunifu nchini.

Tamasha hilo linatarajiwa kuvutia maelfu ya washiriki na kufikia zaidi ya watu milioni moja kupitia majukwaa ya kidigitali, huku taarifa za wasanii watakaoshiriki na ratiba kamili zikitolewa katika siku zijazo.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad