HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, April 10, 2026

NEMC YAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KATIKA USIMAMIZI WA MAZINGIRA UTURUKI

- Yabadilishana uzoefu katika masuala mazima ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira .

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na kufanya mazungumzo na Wizara ya Mazingira, Maendeleo ya Miji na Mabadiliko ya Tabianchi, Taasisi ya Utafiti wa Udongo, Maji na Majanga, Idara ya Maji safi na Maji Taka, Taasisi ya Mradi wa Maendeleo ya Mji wa Konya na Kampuni ya Turko wakati wa maonesho ya zana bora na pembejeo za kilimo na kilimo hifadhi katika Mji wa Konya nchini Uturuki

Mazungumzo hayo yalilenga kubadilishana uzoefu katika masuala ya usimamizi na uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa na kujifunza mbinu bora zinazotumika katika kukabiliana na changamoto za kimazingira.

Akifafanua utekelezaji wa majukumu kutoka NEMC,wakati wa mazungumzo hayo Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi Bi Suzan Chawe amesema wajibu wa Baraza ni kushauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu masuala ya Mazingira na kusimamia Uhifadhi wa Mazingira kwa mujibu wa Sheria na kuainisha majukumu mengine ya Baraza iliyonayo kuwa ni kusimamia mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii, Utafiti wa Mazingira, Uzingatiaji na Utekelezaji Sheria na kutoa elimu ya Mazingira.

Mada zilizojadiliwa ni pamoja na matumizi ya zana zenye kuzingatia kilimo hifadhi, utafiti na utoaji taarifa za kimazingira kwa umma, ushirikishaji wa wadau katika utekelezaji wa Sheria za mazingira, utoaji wa elimu ya mazingira kwa jamii hususani mashuleni, pamoja na mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, wataalam wa Mazingira kutoka Konya walisisitiza umuhimu wa tafiti za kisayansi katika sekta mbalimbali ili kuboresha maamuzi ya kikanuni na kisheria na namna ya kudhibiti uchafuzi unaotokana na shughuli za viwanda.

Mbali na mazungumzo hayo, NEMC pia ilipata fursa ya kutembelea maonesho ya kilimo nchini humo yaliyolenga kuonesha zana zenye kukuza kilimo hifahi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha Maendeleo endelevu yenye kuzingatia usimamizi bora wa mazingira kwa kizazi kijacho.

Ujumbe wa NEMC kutoka Tanzania, ulioambatana na wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wa mazingira , pia ulipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mhe. Iddi Seif Bakari hatua iliyoonesha dhamira ya nchi katika kuimarisha diplomasia ya mazingira na ushirikiano wa kimataifa

Faida za ujio wa NEMC kwenye maonesho hayo pamoja na mazungumzo yaliyofanyika yanatarajia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya NEMC pamoja na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Uturuki katika sekta ya mazingira.










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad