
Na Khadija Kalili, Bagamoyo
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ambao umepokelewa asubuhi tarehe 18 Aprili 2026 kutoka Jijini Dar es Salaam utakagua miradi 68 ambapo kati ya miradi hiyo miradi 23 itawekwa mawe ya msingi, miradi 21 itazinduliwa na miradi 24 itakaguliwa.
RC Kunenge amesema kuwa miradi yote inathamani ya jumla ya Shilingi za Kitanzania Tsh.Bilioni 263,061,799, 595.55.
"Miradi yote hii imefanikiwa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya viongozi wa serikali, wananchi na wadau wa maendeleo" amesema Kunenge.
Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha itaupokea mwenge huo tarehe 20 Aprili 2026 katika shule ya Msingi Gumba kata ya Gwata na kukimbizwa katika Miradi ya Maendeleo na kuhitimishwa kwa mkesha Mkubwa kiwanja cha Shule ya Msingi Mtongani.
Ujumbe mkuu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 , unalenga katika ujenzi wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa chini ya kaulimbiu isemayo 'Tanzania yetu sote , tushikamane kwa kuleta pamoja maendeleo ' kauli mbiu hii inalenga kujenga na kuimarisha umoja wa Kitaifa na kuutumikia Mwenge wa Uhuru kuwaenzi na kuwatia moyo wazalendo wa kweli na makundi mbalimbali yenye mchango mkubwa katika kulinda amani, umoja na mshikamano kitaifa katika kujenga Tanzania imara kimaadili,kidiplomasia na kiuchumi ndani na nje ya mipaka yetu ikiwa ni pamoja na na kurejesha falsafa hii ya Mwenge wa Uhuru kwa wananchi wa Tanzania.
Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Wilaya saba na Halmashauri tisa kwa umbali wa Kilomita 1,065.9

No comments:
Post a Comment