HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 23, 2026

MWANG'ONDA AIPONGEZA RUWASA KWA USIMAMIZI MZURI WA MIRADI YA MAJI KISARAWE-PWANI

Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe Aprili 23, 2026

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameipongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji wilayani Kisarawe mkoani Pwani, ikiwemo mradi wa usambazaji wa maji safi na salama katika vijiji vya Bembeza na Chale, utakaowanufaisha wakazi 2,449.

Pongezi hizo alizitoa wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea, kukagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa maji wa Msanga.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwang’onda alisema Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama, hatua inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, hususan waishio vijijini.

Aidha, aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya mradi huo ili uweze kudumu na kuendelea kuwanufaisha kwa muda mrefu.

Awali, akiwasilisha taarifa ya mradi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kisarawe, Mhandisi Evangelista Kahwili, alieleza mradi huo wenye thamani ya sh.milioni 441.2 umenufaisha wakazi wa vijiji hivyo.

Alieleza kuwa utekelezaji wa mradi ulianza Agosti 30, 2024 na kukamilika Novemba 29, 2025, ukihusisha ujenzi wa mnara wa maji, tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 90,000, vituo tisa vya kuchotea maji pamoja na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa mita 12,820.

Aliongeza kuwa mradi huo umeongeza upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 70.6 hadi 72.8, ukiunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.




 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad