HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 21, 2026

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA KUMUAGA MAREHEMU ASKOFU MFUMBUSA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwasili Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba , Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, kushiriki Ibada ya kumuaga na kumuombea Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, marehemu Askofu Bernadin Francis Mfumbusa, leo tarehe 21 Aprili 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akishiriki Ibada ya kumuaga na kumuombea Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, marehemu Askofu Bernadin Francis Mfumbusa, iliyofanyika Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba , Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, leo tarehe 21 Aprili 2026.





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, marehemu Askofu Bernadin Francis Mfumbusa, mara baada ya Ibada ya kumuaga na kumuombea iliyofanyika Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba , Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, leo tarehe 21 Aprili 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akitoa salamu za rambirambi mara baada ya Ibada ya kumuaga na kumuombea Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, marehemu Askofu Bernadin Francis Mfumbusa, iliyofanyika Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba , Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, leo tarehe 21 Aprili 2026.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Taifa litaukumbuka mchango mkubwa aliyoutoa marehemu Askofu Bernadin Mfumbusa, enzi za uhai wake ikiwemo kuwa kiungo muhimu wa kuunganisha Kanisa Katoliki na Madhehebu mbalimbali pamoja na Dini zingine.

Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kushiriki Ibada ya kumuaga na kumuombea Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, marehemu Askofu Bernadin Francis Mfumbusa, iliyofanyika Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.

Amesema Marehemu Askofu Mfumbusa alijitolea katika kuunganisha dini na madhehebu ili zifanye kazi kwa kuheshimiana, kushirikiana na kupendana. Ameongeza kwamba Taifa litakumbuka mchango wake katika kuhamasisha elimu pamoja na kufanya kazi kubwa ya kuhamasisha na kusimamia ujenzi na uendelezaji wa huduma za Afya katika Wilaya ya Kondoa na Taifa kwa ujumla.

Makamu wa Rais amesema Marehemu Askofu Mfumbusa ametoa mchango katika sekta ya Mawasiliano na Habari akiwa mbobezi na mwalimu katika fani hiyo. Amesema Marehemu Mfumbusa atakumbukwa kwa kutimiza wajibu wake kwa binadamu kwa kutambua Maisha tunayoishi leo, na kutimiza wajibu wake kwa Mungu kwa kutuongoza katika njia ya uzima wa milele.

Aidha Makamu wa Rais amewasilisha salamu za pole za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizotoa kwa Kanisa, Waumini na Familia na kuiombea familia nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Makamu wa Rais amewashukuru Viongozi wa Kanisa Katoliki kwa malezi ya marehemu Askofu Mfumbusa ambayo yalimfanya kuwa mtume wa Taifa zima.

Ibada hiyo, imeongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu Wilbroad Kibozi na kuhudhuriwa na Maaskofu mbalimbali, Mapadre, Watawa, Viongozi mbalimbali wa Serikali na Wananchi.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
21 Aprili 2026
Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad