Madereva wa viongozi mashuhuri (VIP) wa Jeshi la Polisi wametakiwa kuweka mbele jukumu lao la msingi la kulinda maisha ya viongozi wanaowaendesha kwa kuzingatia tahadhari na kuzuia ajali zinazoweza kuepukika, ili kulinda rasilimali watu muhimu kwa taifa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mwezi mmoja kwa madereva wa viongozi hao yanayofanyika chuoni hapo.
Dkt. Mgaya amesema madereva wa VIP wanapaswa kufanya kazi kwa weledi, umakini na nidhamu ya hali ya juu, akisisitiza kuwa viongozi wa juu huandaliwa kwa muda mrefu kwa ajili ya kulitumikia taifa, hivyo kupoteza maisha yao kutokana na uzembe wa madereva ni hasara kubwa kwa nchi.
Aidha, amewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kuyachukulia kwa uzito ili yawaletee mabadiliko chanya na kuwasaidia kupanda madaraja kutoka ngazi za chini hadi za juu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Usafirishaji Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, SACP Fortunatus Muslim, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea madereva ujuzi wa kisasa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya magari yanayotumiwa na viongozi wa juu, jambo litakalosaidia kuongeza usalama barabarani.
Naye Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam na Mratibu wa Mafunzo hayo, DCP Dkt. Lazaro Mambosasa, amewataka madereva kuzingatia viapo vyao vya kazi na kuepuka tabia zisizofaa wanapokuwa kazini.
Ametoa mfano wa baadhi ya vitendo visivyokubalika, ikiwemo madereva kudodondeshea gari upande alipokaa kiongozi wakati wa ajali na kisha kutoweka eneo la tukio, akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi wa kazi hiyo.
Ameongeza kuwa madereva watakaoshindwa kufuzu mafunzo hayo hawatatunukiwa vyeti wala kupandishwa madaraja.
Pia amesisitiza kuwa jukumu la dereva halikomei kumfikisha kiongozi anakoenda pekee, bali linahusisha kujilinda yeye mwenyewe, kuwalinda watumiaji wengine wa barabara pamoja na kulinda magari ya viongozi yanayogharimu fedha nyingi za walipa kodi.










No comments:
Post a Comment