
Taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Kigoma Hilltop Hotel, Ahlulybayt Academic Center, Vision 4 All Eye Centre pamoja na Supa Foam imeendesha kambi maalumu ya siku nne ya matibabu ya macho bure kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma.
Kambi hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 03 hadi 06 Aprili 2026 katika viwanja vya shule za Ahlulbayt Islamic Center Manispaa ya Kigoma Ujiji, ilitoa huduma mbalimbali muhimu ikiwemo uchunguzi wa macho, ushauri wa kitaalamu, utolewaji wa miwani, huduma za dawa pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo.
Akizumza baada ya kukamilika kwa kambi hiyo mlezi wa Taasisi ya LALJI FOUNDATION Mohsen Lalji amesema Zaidi ya wananchi 6000 walijiotokeza kupata huduma ambapo watu 5079 walifanyiwa uchunguzi wa macho, 2218 walipatiwa miwani ya macho, 518 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na watu 3215 walipatiwa dawa za macho huku huduma zote zikitolewa bure bila malipo.
Amesema lengo la kambi hiyo ni kuunga mkono juhudi za serikali na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na endelevu kwa wakati na ukaribu zaidi.
Akizindua rasmi kambi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mh Balozi Simon Sirro aliipongeza LALJI FOUNDATION na washirika wake kwa jitihada hizo za kuwafikia wananchi na kuwapatia huduma muhimu za matibabu ya macho, hususan kwa wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Aidha, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na taasisi zisizo za kiserikali katika kuboresha huduma za kijamii na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Wakizungumza baada ya kupatiwa huduma, wananchi wengi walieleza kuwa walikuwa hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu ya macho, ikiwemo upasuaji na ununuzi wa miwani, hali iliyowafanya kuendelea kuishi na matatizo ya macho kwa muda mrefu.
Wananchi hao pia waliomba juhudi kama hizi ziendelee kudumishwa ili kuwasaidia watu wengi zaidi, hasa wale wa kipato cha chini ambao bado wanakabiliwa na changamoto ya kumudu gharama za huduma za afya.
Kambi hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za wadau wa maendeleo katika kuhakikisha jamii inapata huduma bora za matibabu ya macho hususan katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kama Kigoma.





No comments:
Post a Comment