Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania(TRAMEPRO) Boniventura Mwalongo amekutana na kufanya mazungumzo na Chifu Msangia Ongati Ngoje wa Rorya ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Machifu na Mzee wa Mila na Desturi Mkoa wa Mara.
Kikao hicho kilijikita katika kujadili mustakabali wa taifa letu, hususan katika maeneo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, maadili ya jamii, uadilifu katika utumishi wa umma, pamoja na dira ya maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania.
Taarifa ya Makamu Mwenyekiti wa Machifu na Mzee wa Mila na Desturi Mkoa wa Mara Chifu Msangia Ongati Ngoje amesema katika kikao hicho, wamekubaliana kuimarisha nafasi ya mila na desturi katika utatuzi wa migogoro ya ardhi, kurejesha na kuendeleza maadili na uadilifu katika jamii na taasisi za umma.
Pia kujenga taifa lenye umoja, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali. Aidha, walisisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta ya tiba asili kama nyenzo ya afya na uchumi, na kulinda pamoja na kuendeleza utamaduni wa Waluo kama urithi muhimu wa taifa.
Amesena kama alivyosema mwanafalsafa mashuhuri William Shakespeare, “Ujinga ni laana; maarifa ni mabawa yanayotuinua juu.” ambapo nukuu hiyo inatukumbusha umuhimu wa sayansi, maarifa na elimu katika kuleta maendeleo endelevu ya jamii.
Pia amesema, “Mguso mmoja wa asili huwafanya watu wote kuwa ndugu,” akisisitiza nafasi ya mazingira katika kuunganisha binadamu wote.
Aidha, katika kuelezea maisha ya jamii na utamaduni wake, alisema, “Maisha yetu yamefumwa kwa nyuzi mchanganyiko—mema na mabaya pamoja,” jambo linalotukumbusha wajibu wa kuhifadhi mema ya utamaduni wetu na kurekebisha kasoro zilizopo.
Kwa upande wa uongozi wa kitaifa, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahi kusisitiza kuwa, “Mila na desturi zetu ni utambulisho wetu kama taifa, ni wajibu wetu kuzilinda, kuziheshimu na kuzitumia kama chachu ya maendeleo endelevu.”
Kauli hiyo inaonesha dhamira ya serikali katika kuendeleza urithi wa kitamaduni sambamba na maendeleo ya kisasa.
Kwa upande wa maendeleo ya eneo, Shirati ni Halmashauri ya Mji Mdogo iliyopo katika Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara, Kaskazini mwa Tanzania, karibu na mpaka wa Kenya na kandokando ya Ziwa Victoria.
“Mji huu unakadiriwa kuwa na wakazi kati ya 50,000 hadi 100,000, huku Wilaya ya Rorya ikiwa na takribani wakazi 354,490 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022. Idadi kubwa ya wakazi ni vijana wanaoishi vijijini.
“Shughuli kuu za kiuchumi katika eneo hili ni pamoja na kilimo kinachotegemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wananchi, kikijumuisha mazao ya mahindi, mihogo, mtama, alizeti na pamba.
“Uvuvi pia ni shughuli muhimu inayofanyika katika Ziwa Victoria ukihusisha samaki kama sangara, sato na dagaa. Aidha, wananchi hujihusisha na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo pamoja na biashara ndogo ndogo, ikiwemo biashara za mipakani kati ya Tanzania na Kenya.”
Amesema Kijiografia, eneo la Shirati liko katika Mkoa wa Mara, kaskazini mwa Tanzania, karibu na mpaka wa Kenya na kuzungukwa na Ziwa Victoria, likiwa na hali ya hewa ya kitropiki yenye mvua za msimu. Hali hii huchangia kwa kiasi kikubwa shughuli za kiuchumi na maisha ya wananchi wa eneo hilo.
Amesema utamaduni wa Waluo unaendelea kuwa nguzo muhimu ya mshikamano wa jamii, ukijengwa juu ya heshima kwa wazee na viongozi wa mila, matumizi ya baraza la wazee katika utatuzi wa migogoro, mshikamano wa kifamilia na kijamii, pamoja na kuzingatia maadili ya uadilifu, uwajibikaji na upendo.
Pamoja na hayo amesema ni wazi ushirikiano kati ya viongozi wa mila na desturi, serikali, wataalamu na wananchi ni muhimu katika kujenga jamii yenye maadili imara, uchumi thabiti na maendeleo endelevu.
“Tunatoa mwito kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira, kuendeleza tiba asili, kuhifadhi utamaduni wa Waluo na kutumia vyema fursa zilizopo kwa maendeleo ya Mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla,”amesema Chifu Msangia Ongati Ngoje wa Rorya.


.jpeg)

No comments:
Post a Comment