
MWILI wa marehemu bondia wa zamani wa Taifa, marehemu Lucas Msomba unatarajiwa kuzikwa Jumatatu katika makaburi ya Mkuza yaliyopo Kibaha kwa Mathias mkoani Pwani.
Pichani toka kushoto ni Filbert Bayi (bingwa wa dunia wa mita mbio za 1500), Gidamis Shahanga (bingwa wa marathon wa Jumuiya ya Madola), Emmanuel Mlundwa (bingwa wa ndondi Afrika wa uzito wa flyweight), na Lucas Msomba (bingwa wa ndondi Afrika wa uzito wa lig
Kwa mujibu wa binti wa marehemu, Monica Luca Msomba, ibada ya mazishi itaanza saa nne asubuhi nyumbani kwa familia kilichopo Kibaha kwa Mathias, Mtaa wa Jamaica, barabara ya kuelekea Kambi ya Jeshi Msangani.
Ameeleza kuwa ibada ya nyumbani itafanyika kuanzia saa nne hadi saa tano asubuhi, ambapo ndugu, jamaa na marafiki watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.
Baada ya hapo, mwili wa marehemu utapelekwa Kanisa la Katoliki Mkuza kwa ajili ya ibada ya kuaga itakayofuatiwa na maziko katika makaburi ya Mkuza.
Familia imewaomba waombolezaji kufika kwa wakati ili kushiriki kikamilifu katika ratiba ya mazishi ya mpendwa wao.
Lucas Msomba, bondia wa Taifa maarufu sana miaka ya 80 hadi 90, amefariki dunia siku ya Ijumaa Aprili 10, 2026 huko nyumbani kwake Kibaha kwa Mathias, mkoa wa Pwani.
Msomba, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 72, ni mmoja wa mabondia waliowika sana ndani na nje ya nchi, akiwa na wenzie kina Mlundwa, Habibu Kinyogoli, Nassoro Michael, Isaack Mabushi, Flavian Bitegeko na wengineo.
Licha ya kuwa bingwa wa Taifa kwa muda mrefu, Msomba amekiwakilisha taifa katika mashindano mengi ya ndondi ya uzito wa welterweight ikiwa ni pamoja na Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1980 huko Moscow
Kabla ya hapo, alijipatia heshima kubwa kwa kushinda medali ya shaba katika uzito wa light-welterweight kwenye Michezo ya Afrika ya mwaka 1978 iliyofanyika Algiers.
Msomba anakumbukwa kama miongoni mwa mabondia waliolitangaza sana jina la Tanzania kimataifa, akionesha uwezo, nidhamu na uzalendo mkubwa.
Baada ya kustaafu akawa mshauri kwa mabondia chipukizi, lakini kwa bahati mbaya hakuendelea saakapatwa na maradhi ikabidi akatwe mguu wake wa kuume.


No comments:
Post a Comment