HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 27, 2026

Airtel yazindua mnara wa 4G Mtwara Vijijini, kuongeza upatikanaji wa intaneti Nanguruwe na vijiji jirani

 








Mtwara, Aprili 18, 2026 — Kampuni ya Airtel Tanzania imezindua mnara mpya wa mawasiliano wa 4G katika Kata ya Naguruwe, Wilaya ya Mtwara Vijijini, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za intaneti na mawasiliano katika vijiji vya Nanguruwe na maeneo jirani ambavyo kwa muda mrefu vimekumbwa na changamoto ya mtandao hafifu.

Uzinduzi huo ni sehemu ya mpango wa Airtel wa kupanua huduma zake vijijini ili kuhakikisha jamii zilizo pembezoni zinapata huduma za mawasiliano zenye ubora na uhakika. Vijiji vinavyonufaika na mradi huo ni pamoja na Nanguruwe, Makongoro, Chawi na Mayakuta.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Kanda wa Airtel Tanzania mkoani Mtwara, Saidi Nduguru, alisema uwekezaji huo unalenga kupunguza pengo la kidigitali na kuchochea ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidigitali.

“Mnara huu wa 4G utaongeza ubora wa mawasiliano ya sauti na intaneti, na kuwawezesha wananchi kupata huduma za kidigitali kwa urahisi zaidi, zikiwemo elimu, afya na biashara zinazotegemea mtandao,” alisema Nduguru.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na viongozi wa serikali za mitaa, akiwemo Mtendaji wa Kata ya Naguruwe, Mohamed Chikalangile, ambaye aliipongeza Airtel kwa uwekezaji huo akisema utasaidia kuboresha utoaji wa huduma na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.

Mnara huo unatarajiwa kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo na biashara ndogo ndogo. Katika sekta ya afya, wataalamu wanasema upatikanaji wa mtandao bora utaimarisha mawasiliano kati ya vituo vya afya na kurahisisha rufaa za wagonjwa pamoja na matumizi ya mifumo ya kidigitali ya huduma za afya.

Kwa wakulima, hasa wa zao la korosho ambalo ni tegemeo kuu la uchumi wa eneo hilo, huduma bora za mtandao zitawawezesha kupata taarifa za bei za soko kwa wakati, hali ya hewa na ushauri wa kilimo, jambo linalotarajiwa kuongeza tija na kipato.

Wafanyabiashara wadogo nao watanufaika kupitia huduma za kifedha za simu, malipo ya kidigitali na upatikanaji wa masoko ya mtandaoni, hatua itakayowasaidia kupanua wigo wa biashara zao.

Baadhi ya wakazi wa Nanguruwe wameeleza kufurahishwa na mradi huo wakisema changamoto ya mawasiliano duni imekuwa kikwazo kikubwa kwa muda mrefu, na mara nyingi waliilazimika kusafiri hadi mjini kupata huduma za intaneti.

“Tumekuwa na changamoto ya mtandao hafifu kwa muda mrefu. Sasa tutapata fursa za mawasiliano na biashara ambazo zilikuwa ngumu kufikiwa,” alisema mkazi wa Nanguruwe, Patrick Simunga.

Asia Hamisi, mkazi mwingine, alisema maboresho hayo yatafungua fursa mpya za kiuchumi ikiwemo upatikanaji rahisi wa huduma za kifedha kupitia simu na taarifa za biashara.

Airtel Tanzania imesema inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano nchini, hususan maeneo ya vijijini, kama sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanaunganishwa na uchumi wa kidigitali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad