HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 13, 2026

WIZARA YA NISHATI, PURA WAWEKA MIKAKATI KUIMARISHA UTAFUTAJI WA MAFUTA, GESI ASILIA NCHINI

Wizara ya Nishati kupitia Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi asilia Dkt. James Mataragio imekutana na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Kikao hicho kilichofanyika Machi 12, 2026 Jijini Dar es Salaam kilihudhuriwa na Kamishna Msaidizi wa Petroli kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Antelimi Raphael, Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni na baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Nishati na PURA.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Dkt. Mataragio alieleza kuwa miongoni mwa masuala yanayohitaji kufanyiwa kazi kubwa katika sekta ya mafuta na gesi ni eneo la utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini kwa kuzingatia kuwa shughuli hizo zimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Miaka ya nyuma, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini zilikuwa zikifanyika kwa wingi na kasi kubwa. Tukiangalia hata mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato yani PSA, zilikuwa zaidi ya 26 lakini leo hii tunaongelea mikataba 11 pekee”

“Na ukijaribu kuangalia kwa kina, hata katika PSA zilizobaki, ni kampuni chache zinatekeleza majukumu yao ya kuendelea kufanya utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Hali hili hairidhishi. Lazima tuweke mikakati inayolenga kuchochea shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini” alisema Dkt. Mataragio.

Alibainisha kuwa mdororo wa shughuli za utafutaji ni hatari kwa uhakika wa upatikanaji wa gesi asilia kwa kuwa utafutaji ndio chachu ya ugunduzi ambao ukiendelezwa unapelekea uzalishaji wa gesi asilia.

“Kwa sasa tumejipanga kama Wizara kuhakikisha tunaweka jitihada kubwa katika eneo hili na kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia” aliongeza Dkt. Mataragio.

Kwa upande wake, Mha. Charles Sangweni alieleza kuwa PURA imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuingia mikataba na makampuni ya kijiofizikia yaliyobobea katika ukusanyaji wa data za petroli (Multi Client Geophysical Companies) kwa lengo la kuendeleza utafiti katika maeneo ya bahari kuu na nchi kavu.

Kupitia kikao hicho, Wizara ya Nishati na PURA zilijadili kwa kina mikakati ya kuimarisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia na kuainisha masuala muhimu yanayopaswa kufanyiwa kazi haraka ili kuleta uhai katika sekta.
  


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad