HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 27, 2026

WAVUVI ACHENI KUPUUZA MATUMIZI YA VIFAA OKOZI-DC HAULE

 

Mkuu wa Wilaya ya Rorya Dkt. Khalfany Haule  akizungumza na maafisa wa TASAC waliotembelea Ofisi ya Mkoa wa Mara hawapo pichani.
Afisa Mfawidhi wa TASAC mkoa wa Mara Mhandisi Hezron Lusangija akitoa elimu ya usalama majinI kwa   Wavuvi wa Wilaya ya Rorya.


*Jaketi Okozi ni Uhai na sio mzigo kwa msafirishaji

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Wilaya ya Rorya imetoa wito kwa wavuvi na wamiliki wa mitumbwi kuacha kupuuza matumizi ya vifaa vya kuokoa maisha majini.

Hayo ameyasema Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mhe. Dkt. Khalfany Haule wakati maafisa Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) walipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kutoa elimu ya Usalama wa vyombo vya majini.

Dkt. Haule alionya dhidi ya mtazamo potofu kwamba maboya ni mzigo wa gharama na kikwazo cha kazi ya uvuvi

Amesema kwa takwimu za mwaka uliopita, zaidi ya wavuvi 20 walipoteza maisha kutokana na mitumbwi kuzama, licha ya kuwa na maboya ndani ya vyombo lakini bila kuyavaa.

"Kupoteza maisha ni pigo kubwa kwa familia na inapunguza nguvu kazi ya taifa” amesema Mhe.Dkt.Haule

Afisa Mfawidhi wa TASAC mkoa wa Mara Mhandisi Hezron Lusangija, aliongeza kuwa wavuvi wengi hujiamini kupita kiasi kwa kudhani ujuzi wa kuogelea unatosha, jambo linalowaweka hatarini. Kwa sasa ni msimu wa upepo mkali, mawimbi makubwa na mvua zinazoendelea kunyesha zimeongeza hatari ya ajali majini.

Kwa kukabiliana na hilo, TASAC imeanzisha kampeni ya kutoa elimu kwa wamiliki wa vyombo vidogo, wavuvi, vyama vya wamiliki na wananchi ili kuondoa mitazamo potofu, tabia ya kupuuza na kuimarisha usalama wa usafiri majini.

Mhandisi Lusangija aliongeza kuwa wavuvi na wasafirishaji wajenge utamaduni wa kufuatilia utabili wa hali hewa kuliko kutumia utaalam wa asili, watumie mialo rasmi na kuwa na maboya.

Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa mitumbwi, akiwemo Hamza Kisuki, wamelalamikia tabia ya wavuvi kuvua maboya mara wanapofika majini na kuyageuza kuwa mito ya kulalia, wakijiamini kuwa uwezowao wa kuogelea unatosha.

Elimu hii imeanza kutolewa katika mwalo wa Esegere na Nyang’ombe, na itaendelea katika mialo ya Kinesi, Sota, Luhu, Busanga na Kilongwe. Walengwa ni viongozi wa Serikali za Mitaa, BMU, wavuvi, wamiliki wa mitumbwi na wananchi kwa ujumla.
Afisa Mfawidhi wa TASAC mkoa wa Mara Mhandisi Hezron Lusangija akitoa elimu kwa mvuvi namna ya kuvaa jaketi Okozi wakati wa dharula ya hatari.
Wavuvi na wamiliki wa Mitumbwi wakipata elimu ya usalama majini kutoka kwa maafisa wa TASAC hawapo pichani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad