
Watumishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Makao Makuu wamepatiwa mafunzo maalum ya lishe pamoja na mwongozo wa kudhibiti VVU/ UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwaimarisha kiafya na kuongeza ufanisi wao kazini.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika tarehe 27 Machi, 2026 katika ofisi za wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, yakilenga kuwajengea watumishi uelewa mpana kuhusu namna bora ya kujikinga na magonjwa pamoja na kuzingatia lishe bora katika maisha ya kila siku.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Bw. Deodatus Mwiliko, alisema kuwa afya ya mtumishi ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija na ufanisi kazini, hivyo ni muhimu kwa watumishi kupewa elimu sahihi ya afya mara kwa mara.
Alieleza kuwa, Wizara ya Ardhu, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imejipanga kuhakikisha watumishi wake wanapata mafunzo mbalimbali yanayogusa ustawi wao, ikiwemo masuala ya afya, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Katika mafunzo hayo, mada kuhusu mwongozo wa kudhibiti VVU/UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa iliwasilishwa na Bi. Juliana Ntukey kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuzingatia miongozo iliyopo ili kulinda afya za watumishi na jamii kwa ujumla.
Aidha, mada ya lishe bora iliwasilishwa na Bi. Semeni Eva Juma, Afisa Lishe kutoka Jiji la Dodoma, ambapo alitoa elimu juu ya umuhimu wa kula mlo kamili na wenye virutubisho vinavyohitajika kwa afya bora ya mwili.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yamepokelewa kwa hamasa kubwa na watumishi, huku yakitarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika kuimarisha afya na ustawi wao mahali pa kazi.

Bi. Juliana Ntukey kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi akitoa mafunzo kuhusu muongozo wa kudhibiti VVU/Ukimwi na magonjwa sugu zyasiyoambukizwa kwa watumishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi jijini Dodoma tarehe 27 Machi 2026.



Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakiwa katika mafunzo maalum ya lishe pamoja na mwongozo wa kudhibiti VVU/UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 27 Machi, 2026.
Bi. Juliana Ntukey kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi akitoa mafunzo kuhusu muongozo wa kudhibiti VVU/Ukimwi na magonjwa sugu zyasiyoambukizwa kwa watumishi wa Wizara ya Ardhi Jijini Dodoma tarehe 27 Machi 2026.






No comments:
Post a Comment