HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 16, 2026

WANANCHI WA MOHORO WAMSHUKURU RAIS SAMIA


-Mhe. Mchengerwa afuturisha, Mohoro, Chumbi,Mbwala na Shela

-Maelfu ya wananchi washiriki futari, wamsifu Mchengerwa

Na Yohana Kidaga- Mohoro

Wananchi wa kata nne za Muhoro, Chumbi, Mbwala na Shela katika wilayani Rufiji wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye tukio maalum la kuwafuturisha wananchi wa kata hizo Machi 15, 2026 lililofanywa Mbunge wa Rufiji na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambapo takribani wananchi elfu kumi walishiriki kutoka katika kata hizo wamesema katika kipindi hiki chini ya Rais Samia miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa, hali ambayo imeleta mabadiliko makubwa.


“Ukweli lazima usemwe, ni katika kipindi hiki ambapo tunaishukuru Serikali yetu, kwa uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais ambapo ameweza kutusimamia na kupitia mbunge wetu ambaye amekuwa na moyo wa kizalendo na upendo na sisi watu wake, miradi kwenye sekta zote imeendelea kutekelezwa”. Alisema Abdul Bakari Chobo ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji na Diwani wa Kata ya Mohoro.

Akizungumzia suala la ujenzi wa barabara katika jimbo hili Mhe. Chobo alifafanua kwamba tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye mtandao wa wa zaidi ya kilomita 20 kwa kiwango cha lami na amesisitiza kuwa kata zote zinakwenda kuunganishwa kwa barabara.

Aidha, amesema katika kipindi cha sasa tayari Serikali imeshaleta takribani shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kukarabati hospitali ya Wialaya ya Utete, Kituo cha Afya cha Mkongo,na zahanati kadhaa katika wilaya ya Rufiji.


Kabla ya kuanza kufuturisha, Mhe. Mchengerwa pia alimshukuru Mhe. Rais kwa niaba ya wanachi kwa kuwaletea wananchi maendeleo ambapo alisema Serikali imefanya maboresho makubwa siyo tu katika eneo la miundominu ya barabara bali ujenzi wa madaraja makubwa yanayoiunganisha Rufiji na mikoa mbalimbali, ujenzi wa Shule za Sekondari na Msingi, Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali na kuleta watumishi wa kutosha.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kwenye matukio ya kufuturu yanayoendelea katika jimbo lake huku akifafanua kuwa mwitikio huo ni ishara ya upendo mkubwa walionao kwake na Serikali yao, kwani kama wasingekuwa na imani na yeye hata kama angewaandalia futari wasingeweza kushiriki.

“Natambua watu wameacha kazi zao kwa ajili ya kuja kushiriki kwenye futari hii, huu ni upendo mkubwa sana kwangu binafsi na Serikali yao, pia wamenithibitishia maamuzi waliyoyafanya wakati wa kupiga kura za ubunge na urais ambapo walinichagua kwa kura za kishindo mimi na chama changu.” Jambo hili linanifanya niwe na deni kubwa kwao la kuendelea kuwatumikia, naahidi kufanya hivyo kwa moyo wangu wote” alifafanua Mhe. Mchengerwa.

Akizungumzia msingi wa uongozi bora Mhe. Mchengerwa alisitiza viongozi kushuka chini kwa wananchi na kuwatumikia wananchi kwa katika kipindi chote ili kuwaletea maendeleo ya kweli badala ya kusubiri vipindi vya kampeni pekee.

Ni vizuri kama kiongozi mwenye dhamana kushuka chini kushirikiana na wananchi katika ambapo amesema katika kipindi chake amekuwa nyakati zote na wananchi ili kuhakikisha ahadi ambazo amezitoa kwa kushirikiana na wananchi wanakwenda kuzitekeleza kwa manufaa na maendeleo ya wananchi.

Ikiwa ni mwendelezo wa mwaka wanne mfululizo wa kuwafuturisha wananchi wa jimbo la Rufiji leo Machi 16, 2026 Mhe. Mchengerwa anakusudia kuendelea kufuturisha katika kata ya Mwaseni baada ya jana kufuturisha kata nne za Muhoro, Chumbi,Mbwala na Shela katika eneo la Muhoro ,kabla ya juzi kufuturisha katika eneo la Utete.


Katika hatua nyingine, mbali na kuwafuturisha wananchi hao,Mhe. Mchengerwa alipata fursa ya kuwasikiliza wananchi mmoja mmoja na kutoa ufumbuzi wa changamoto zao ambapo wananchi waliopata fursa walipongeza hatua hiyo.

“Tunampongeza mbunge wetu kwa kutuandalia futari katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na pia Kwaresma kwani inatuunganisha sisi sote, hii ni alama ya upendo na kwa kweli tunapata fursa ya kukutana na kiongozi wetu na kujadiliana naye mambo mbalimbali na anatutatulia hapo hapo huu ndiyo uongozi”. Alisema Ayubu Issa Mkazi wa Mohoro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad