Afisa Uwekezaji Mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Mitaji (UNCDF) , Bw. Abraham Byamungu (wa kwanza kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Afisa wa Misitu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Lucas Jacob Sabida wakati wa warsha ya kujadili sera zinazohusiana na biashara ya kaboni iliyofanyika katika Hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam
Afisa Uwekezaji Mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Mitaji (UNCDF) , Bw. Abraham Byamungu (kulia) akichangia mada katika warsha ya kujadili sera zinazohusiana na biashara ya kaboni iliyofanyika katika Hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam jana kushoto ni Meneja Mkaazi wa VPenergy Tanzania Bi. Jacqueline Ngulla.
Afisa Uwekezaji Mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Mitaji (UNCDF) , Bw. Abraham Byamungu (katikati) akiteta jambo na mtaalamu wa biashara ya Carbon Bi. Annika Richter (kushoto) na mtaalamu wa nishati kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Program-WFP) Dkt. Geoffrey Ndegwa katika warsha ya kujadili sera zinazohusiana na biashara ya kaboni iliyofanyika katika Hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Mitaji (UNCDF), kupitia programu ya nishati safi (Clean Cooking- CookFund” inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), limeandaa majadiliano ya sera yaliyowakutanisha wadau muhimu wakiwemo Wizara ya Nishati, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT), Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni ( NCMC), wataalamu wa masoko ya kaboni, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo, kujadili fursa na changamoto katika kuendeleza biashara ya kaboni nchini Tanzania.
Afisa Uwekezaji Mwandamizi wa UNCDF Bw.Abraham Byamungu, amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika biashara ya kaboni, sekta inayosaidia kupunguza uzalishaji wa gesi chafu duniani kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo miradi ya ufanisi wa matumizi ya nishati, utekelezaji wa Mkakati wa Taifa unaolenga kuwahamasisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, pamoja na uhifadhi wa misitu.
Akizungumza wakati wa majadiliano yenye mada *“Kuimarisha Ustahimilivu wa Udhibiti na Kuongeza Imani ya Wawekezaji katika Mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia Inayotegemea Kaboni,” yaliyofanyika katika Hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam jana, Bw. Byamungu alisema kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuweka mazingira bora ya uwekezaji na sera zitakazoiwezesha sekta hiyo kuwanufaisha Watanzania kwa kiwango kikubwa zaidi.
Alieleza kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuvutia wawekezaji katika sekta ya biashara ya kaboni. Hata hivyo, alisema nchi bado ipo nyuma ikilinganishwa na baadhi ya nchi za ukanda huu kama Rwanda, ambayo licha ya kuwa na eneo dogo kijiografia imefanikiwa kupiga hatua kutokana na maandalizi mazuri, mazingira rafiki ya uwekezaji na sera zinazounga mkono ukuaji wa biashara hiyo.
Aidha, alitaja nchi jirani ya Kenya kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa katika biashara ya kaboni kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali na kuweka sera zinazowezesha ukuaji wa sekta hiyo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kuzidi nchi nyingi barani Afrika kutokana na ukubwa wa ardhi yake, jitihada zinazoendelea katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, pamoja na ukweli kwamba takribani asilimia 34 ya ardhi ya nchi imehifadhiwa kama misitu na maeneo ya wanyamapori, jambo linalotoa fursa kubwa za biashara ya kaboni kupitia upandaji miti na uhifadhi wa misitu.
Katika kuhakikisha biashara ya kaboni inanufaisha nchi, alisema UNCDF inaendelea kuwakutanisha wadau kwa kuandaa majukwaa mbalimbali yanayowaunganisha wataalamu wa sekta hiyo ili kutoa elimu na mwongozo kuhusu namna ya kunufaika na fursa za biashara ya kaboni.
“Lengo letu ni kuwa na majukwaa ya pamoja ambapo tunaweza kujadiliana na kushirikishana uzoefu kutoka nchi nyingine ili tujifunze na kufanya vizuri zaidi,” alisema.
Kwa upande wake, Bw. Lucas Jacob Sabida, Afisa Misitu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, alisema warsha hiyo ni muhimu kwa kuwa inaleta pamoja wadau mbalimbali kujadili namna biashara ya kaboni inavyoweza kuinufaisha Tanzania kama ilivyofanya katika baadhi ya nchi jirani.
Alisema Serikali, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, iko tayari kusaidia ukuaji wa soko la kaboni kupitia Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Biashara ya Kaboni (NCMC) ambacho kimeanzishwa kusaidia kuandaa sheria, miongozo na kanuni mbalimbali ili kuhakikisha nchi inanufaika kikamilifu na biashara hiyo.
Aliongeza kuwa Serikali tayari imeweka mazingira mazuri ya kukuza sekta hiyo kwa kuanzisha NCMC, kituo kinachoratibu masuala yote yanayohusiana na biashara ya kaboni ikiwemo usajili wa miradi, ili kuhakikisha sekta hiyo inakua na kuleta manufaa kwa taifa.
“Tunawapongeza sana UNCDF kwa kuandaa mikutano kama hii ambayo inatupa fursa ya kujadili kwa pamoja namna biashara ya kaboni inaweza kuleta matokeo chanya nchini,” alisema Bw. Sabida.
“Tunao imani kuwa kupitia ushirikiano huu kati ya Serikali na sekta binafsi tutapata mafanikio makubwa katika biashara ya kaboni,” aliongeza.
Pia alieleza kuwa Serikali iko tayari kupitia sera ambazo zinaweza kuwa kikwazo kwa maendeleo ya sekta hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuweka mazingira bora zaidi kwa ukuaji wa biashara ya kaboni nchini.
Katika kuhitimisha majadiliano hayo, wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo walikubaliana kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha jitihada za pamoja zinatumika kuongeza manufaa ya biashara ya kaboni kwa Tanzania.
Walisisitiza kuwa uratibu mzuri na mshikamano kati ya wadau ni muhimu ili kuhakikisha biashara ya kaboni inachangia ukuaji wa uchumi wa nchi huku ikilinda mazingira kupitia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na usimamizi endelevu wa misitu na ardhi.




No comments:
Post a Comment