HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 26, 2026

AXA, Alliance na MIC Global Kuimarisha Huduma za Afya za Nje ya Nchi

 

Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wanatarajiwa kunufaika na huduma za afya za kimataifa kufuatia ushirikiano wa kimkakati kati ya AXA Health International, Alliance Insurance Corporation Limited na MIC Global Risk Tanzania Ltd, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa bima ya afya ya kimataifa pamoja na matibabu maalum nje ya nchi.

Kupitia ushirikiano huo, kampuni hizo tatu zimeunganisha utaalamu wao ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya za kiwango cha juu kwa watu binafsi, wafanyabiashara, wageni wanaoishi nchini pamoja na wataalamu wanaosafiri kimataifa. Mpango huo unawawezesha wateja kupata matibabu maalum katika hospitali za nje ya nchi pale inapohitajika kupitia bima ya afya ya kimataifa.

Hatua hiyo inakuja kufuatia ushirikiano wa AXA Health International na Executive Healthcare Solutions ulioanzishwa Oktoba 2025 kwa lengo la kuimarisha mfumo wa usambazaji wa huduma za bima ya afya ya kimataifa nchini Kenya na maeneo mengine ya Afrika. Nchini Tanzania, MIC Global Risk Tanzania Ltd imechaguliwa kuwa msambazaji wa kipekee wa huduma hizo katika soko la ndani kwa kushirikiana na Alliance Insurance Corporation Limited.

Kupitia mpango unaojulikana kama Global Executive Health Plan (GEHP), wateja watapata fursa ya kufikia mtandao mpana wa hospitali na wataalamu wa afya wanaotambulika kimataifa, pamoja na huduma za ziada kama uokoaji wa kimatibabu na uratibu wa matibabu yanayofanyika nje ya mipaka ya nchi.

Akizungumzia ushirikiano huo, Afisa Mkuu wa Uendelezaji wa Biashara wa AXA Global Healthcare, Karim Idilby, amesema kuanzishwa kwa huduma hiyo nchini Tanzania ni hatua muhimu katika mkakati wa kampuni hiyo kupanua uwepo wake katika masoko yenye ukuaji wa haraka barani Afrika.

Amesema kadri Tanzania inavyoendelea kuwa kitovu cha uwekezaji, biashara na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, ndivyo mahitaji ya huduma za afya za kimataifa yanavyozidi kuongezeka, jambo linalofanya ushirikiano huo kuwa na umuhimu mkubwa kwa wateja wanaohitaji matibabu maalum nje ya nchi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Alliance Insurance Corporation Limited, Rajiv Kumar, amesema ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kuongezeka kwa watu wanaosafiri kimataifa kumeongeza mahitaji ya huduma za afya za kimataifa zilizo salama na zinazoaminika.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa MIC Global Risk Tanzania Ltd, Aly Maherali, amesema mpango wa GEHP unaunganisha uzoefu wa kimataifa wa AXA Global Healthcare na mfumo wa bima ya ndani unaosimamiwa na Alliance Insurance Corporation Limited, hatua inayowapa watu binafsi, makampuni na wataalamu nchini Tanzania fursa ya kupata ulinzi wa afya katika kiwango cha kimataifa.

Amesema kwa zaidi ya miaka 25 kampuni yake imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa bima ya afya ya kimataifa katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, na ushirikiano huo unaimarisha dhamira ya kuendelea kuwahudumia wateja nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.












Matukio mbalimbali katika Picha.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad