Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara alioufanya katika viwanja vya Stendi ya zamani, akibainisha kuwa kumekuwa na miradi mingi iliyoanzishwa ndani ya wilaya hiyo inayoelezwa kuwa ni miradi ya wananchi lakini badala yake imegeuka kuwa miradi binafsi ya watu akitolea mfano wa mradi wa kiwanda cha matofali uliohoji juu ya uwepo wake na kudai kuwa ulibaki kuwa mali ya watu wawili kabla ya mradi husika kufa.
Awali Miongoni mwa hoja zilizoibuliwa na wananchi kupitia mkutano huo ni pamoja na changamoto ya maji yanayotoka bombani kuwa machafu hali inayohatarisha afya za watumiaji,ombi la kuwekwa kwa matuta katika barabara kuu ili kudhibiti ajali hususani katika nyakati za jioni kutokana na msongamano wa watu,ombi la ujenzi wa soko la Chato,uwepo wa changamoto katika soko la wamachinga Kitera,bima ya Afya kwa wazee na ujenzi wa chuo kikuu pamoja na changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA.
Akijibu hoja hizo,Mbunge Magembe ameeleza kwamba atahakikisha vyote vilivyoanzishwa na mtangulizi wake katika Jimbo hilo Hayati Dkt.John Pombe Magufuli vitatekelezwa akieleza kwamba wale wote wasio na mapenzi mema na Chato na kutaka kuipeleka wilaya hiyo shimoni hatokuwa tayari kuwa nao na kubainisha kuwa ataendelea kushirikiana na madiwani walio tayari kutanguliza maslahi ya wananchi waliowapigia kura badala ya kutanguliza maslahi yao binafsi.
Kuhusiana na changamoto ya barabara ameeleza kuwa barabara za kuingia hospitali ya rufaa ya Kanda ya Chato na barabaraba za Chato mjini tayari barabara mbili zipo katika hatua ya ujenzi katika kipindi ambacho Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC) unaotarajiwa kuwezesha ujenzi wa soko kubwa la Muungano kwa kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 53 na barabara zenye urefu wa kilomita 10 kwa kiwango cha lami ndani ya mji huo.
Pia ameelezea uwepo wa mkakati wa ujenzi wa mfereji wa kuzuia mafuriko na kuahidi kuwasilisha kwa Meneja wa TANROADS ombi la ujenzi wa matuta ya kudhibiti ajali barabarani na kueleza kwamba changamoto ya vitambulisho vya Taifa ataifikisha kwa mkuu wa wilaya ili kuhakikisha wahusika wanawafuata wananchi mitaani na kuwapatia huduma ya uandikishaji na kuwaondolea kero hiyo.
Aidha kupitia mkutano huo,Mbunge huyo pia amegawa jezi na mipira kwa vijiji vine vinavyounda kata ya Chato ukiwa ni mwendelezo wa kutoa vifaa vya michezo katika vijiji zaidi ya 60 vilivyopo ndani ya Jimbo la Chato Kaskazini.

No comments:
Post a Comment