04 MACHI, 2026 ZANZIBAR
*ZASISITIZA USHIRIKIANO MAENEO YA UTAALAMU, UZOEFU
NAIBU Katibu Mtendaji Tume ya Haki za binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Juma Msafiri Karibona amehimiza suala la ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Tume hiyo kwa ofisi za Unguja na Pemba.
Bw. Karibona aliyasema hayo ofisi za Tume zilizopo Mombasa, Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi alipozungumza katika kikao cha pamoja kilichowashirikisha watumishi wa THBUB ofisi ya Unguja na Pemba kwa njia ya mtandao (zoom meeting).
Aidha, Bw. Karibona alisisitiza ushirikiano zaidi katika kubadilishana uzoefu na utaalamu huku akiisifia THBUB ofisi ya Pemba kupiga hatua zaidi katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo ufunguzi wa klabu za haki za binadamu katika taasisi za elimu kwa skuli na vyuo vya kati pia kufanikiwa kutembelea maeneo ambako watu huzuiliwa kama vituo vya kulelea watoto yatima na kufanya vipindi mbalimbali katika vyombo vya habari ili kuifikia jamii kwa haraka na kuwapa elimu ya Haki za Binadamu na Ukiukwaji wa Misingi ya Utawala Bora.
Katika hatua nyengine Bw. Karibona alimsihi Mfawidhi wa ofisi ya Pemba Bw. Suleiman Salim Ahmad, kuwatumia wataalamu waliopo ofisi ya Unguja na kuangalia namna bora ya kuboresha bajeti za ofisi hizo.
Alisema, licha ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa na ofisi mbili hizo ikiwemo ongezeko la rasilimali watu kutoka wafanyakazi nane hadi 26 kwa ofisi ya Unguja na Pemba kutoka wafanyakazi wawili hadi wafanyakazi nane.
Pia Bw. Karibona alitaja maeneo muhimu zaidi ya kuimarisha ushirikiano wao ni eneo la Elimu kwa Umma na masuala ya habari, Utumishi, Utawala, Uhasibu na eneo la Mipango.
Naye, Mfawidhi wa THBUB ofisi ya Pemba Bw. Suleiman Salim Ahmad alikiri kuwa Pemba imeitangulia Zanzibar katika utekelezaji wa kazi zao ikiwemo ufunguzi wa klabu ambapo kwa sasa tayari wameshafungua klabu 15 za Haki za Binadamu kwa taasisi za elimu zikiwemo mbili kwa skuli za msingi, saba Sekondari na sita kwa vyuo vya kati.
Aidha, viongozi wawili hao wamekubaliana kuimarisha bajeti za ofisi zao katika kuwatumia wataalamu waliopo Unguja na kuendeleza utendaji kazi wa ofisi za Tume kisiwani Pemba.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment