HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 24, 2026

TANZANIA YAONGEZA KASI KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU; WITO WA USHIRIKIANO WATOLEWA



Na John Mapepele

Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amesema Tanzania leo, Machi 24, 2026 imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani, siku maalum inayolenga kuongeza jitihada za kupambana na ugonjwa huu hatari unaoendelea kuathiri mamilioni ya watu duniani.

Amewataka watanzania kuendelea kushirikiana na Serikali ili kutokomeza ugonjwa huo hapa nchini.

"Ili kuhakikisha tunafanikiwa kutokomeza ugonjwa huu, jitihada za pamoja za wadau wote katika kuwajibika zinahitajika." Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Aidha, katika tamko rasmi lililotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, Serikali imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kufanikisha azma ya kutokomeza kifua kikuu ifikapo mwaka 2030.

Kauli mbiu ya mwaka huu, “Kwa Jitihada za Pamoja za Viongozi, Wadau na Wananchi, inawezekana Kutokomeza Kifua Kikuu nchini,” imebeba ujumbe mzito wa uwajibikaji kwa kila mmoja.

Kauli hii inalenga kuwakumbusha viongozi, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi kuwa mapambano dhidi ya kifua kikuu yanahitaji mshikamano na mchango wa pamoja, ikiwemo uwekezaji wa rasilimali kutoka ndani ya nchi.

Licha ya ugonjwa huu kubaki kuwa miongoni mwa magonjwa hatari ya kuambukiza, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza maambukizi mapya.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2024, visa vya kifua kikuu vimepungua kwa asilimia 44—kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi 172 kwa mwaka 2024. 

Aidha, vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vimepungua kwa asilimia 59, kutoka vifo 56,000 hadi 23,500 katika kipindi hicho.

Mafanikio haya yanachangiwa na uwekezaji wa Serikali katika sekta ya afya, hasa kuboresha miundombinu ya uchunguzi na upatikanaji wa dawa.

Serikali pia imehakikisha wagonjwa wanapatiwa matibabu bila malipo na kufuatiliwa ili kuhakikisha wanamaliza dozi, hatua muhimu katika kuzuia usugu wa dawa.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, bado juhudi zinahitajika ili kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa huu ifikapo mwaka 2035.

Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima mapema wanapopata dalili kama kikohozi cha muda mrefu, homa za mara kwa mara, jasho la usiku au kupungua uzito.

Aidha, jamii imetakiwa kuondoa unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa kifua kikuu na badala yake kuwapa msaada wa kijamii na kisaikolojia. 



Dkt. Magembe amesisitiza kuwa mgonjwa anapoanza matibabu hupunguza uwezekano wa kuambukiza wengine, hivyo ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kudhibiti maambukizi.

Katika kukabiliana na ugonjwa huu, wananchi pia wanahimizwa kuzingatia tahadhari kama kuepuka msongamano usio wa lazima, kuhakikisha maeneo yenye hewa safi na kutoa taarifa mapema kwa wahudumu wa afya kuhusu watu wenye dalili.

Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeahidi kuendelea kuboresha huduma za afya hadi ngazi ya jamii ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora kwa wakati.

Serikali inatoa wito kwa Watanzania wote kuchukua hatua ambapo kwa kufanya hivyo kutasaidia kutokomeza kifua kikuu na kulinda afya ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad