HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 5, 2026

SHEIKH MKUU WA TANZANIA AWAHAMASISHA WANAWAKE KUMILIKI ARDHI BAADA YA KUPATA HATI SAMIA ARDHI KLINIKI

Dar es salaam – 05/03/2026

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kutumia fursa ya huduma za ardhi zinazotolewa kupitia Samia Ardhi Kliniki, akisisitiza umuhimu wa wanawake kumiliki ardhi kama njia ya kujikomboa kiuchumi.

Mufti Zubeir alitoa kauli hiyo baada ya kufika katika Kliniki ya Ardhi inayofanyika katika Ofisi za Ardhi za Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo alipata hati ya ardhi huku akishuhudia namna wananchi wanavyohudumiwa katika kliniki hiyo ambayo inaendelea nchi nzima.
Akizungumza mara baada ya kupata huduma hiyo, Mufti Zubeir alisema hatua ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuandaa Samia Ardhi Kliniki yenye kulenga kuwapa kipaumbele wanawake ni jambo muhimu linalosaidia kuongeza usawa katika umiliki wa rasilimali muhimu kama ardhi.

Alisema wanawake wanapaswa kutumia kikamilifu fursa hiyo ili waweze kupata hati za ardhi na kujiimarisha kiuchumi.

“Wanawake wana haki ya kumiliki mali mbalimbali ikiwemo magari na mali nyingine, hivyo hakuna sababu ya kuwanyima nafasi ya kumiliki ardhi. Ni muhimu jamii, hususan wanaume, kuachana na mila kandamizi zinazowazuia wanawake kumiliki rasilimali,” alisema Mufti Zubeir.

Aidha, aliwataka wanaume kuwapa nafasi wanawake kumiliki ardhi ili kuongeza idadi ya wanawake wenye umiliki rasmi wa ardhi nchini, jambo ambalo litasaidia kuimarisha ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Mufti Zubeir alipongeza maandalizi mazuri yaliyofanywa na Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam katika uendeshaji wa kliniki hiyo, kuanzia mapokezi hadi utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alisema namna wateja wanavyohudumiwa kwa ufanisi ni jambo jema lenye manufaa kwa jamii na lina thawabu kubwa mbele za Mwenyezi Mungu, hususan katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mufti Zubeir pia aliwaombea heri watumishi wanaotoa huduma katika kliniki hiyo ili waendelee kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na bidii.

Samia Ardhi Kliniki zinaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi, hususan kwa wanawake, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka.



 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad