HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 23, 2026

SEKTA YA MAZIWA YAPATA NGUVU MPYA: WAKAGUZI WAPEWA MAFUNZO MOROGORO

Sekta ya maziwa nchini imepata msukumo mpya kufuatia kuanza kwa mafunzo maalum kwa wakaguzi wa maziwa kutoka mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Pwani yanayofanyika mkoani Morogoro kwa siku Tatu, yakilenga kuimarisha ubora, usalama na ushindani wa bidhaa za maziwa katika soko la ndani na nje ya nchi.

Akifungua rasmi mafunzo hayo Machi 23, 2026 yanayofanyika katika Ukumbi wa Savoy mkoani Morogoro, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Prof. George Msalya, alisema kuwa mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha wakaguzi wanakuwa na ujuzi wa kisasa wa kusimamia viwango vya ubora wa maziwa kuanzia uzalishaji hadi kwa mlaji.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta hiyo ili kulinda afya za wananchi na kuongeza thamani ya maziwa yanayozalishwa nchini.

Awali, akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Afisa Mifugo wa Mkoa wa Morogoro, Bw. David Mahimbo, alisema kuwa mafunzo hayo yanakuja wakati muafaka ambapo mkoa huo unaendelea kuimarisha uzalishaji wa maziwa.

Alieleza kuwa uwepo wa wakaguzi wenye ujuzi utasaidia kudhibiti ubora wa maziwa na kuongeza imani ya walaji pamoja na masoko ya bidhaa za maziwa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi.Mariam Kingu, wakati akitoa salamu za Wizara kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko (DPMD), alieleza kuwa Wizara inaendelea kushirikiana na Bodi ya Maziwa Tanzania katika kuboresha sekta hiyo kupitia sera, miongozo na programu za mafunzo.

Alisisitiza umuhimu wa wakaguzi kuwa na weledi na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha maziwa yanayofika kwa walaji ni salama na yenye viwango vinavyokubalika.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwaongezea wakaguzi uelewa wa masuala ya udhibiti wa ubora, usafi wa maziwa, na utekelezaji wa sheria na kanuni za sekta ya maziwa, hatua itakayochochea ukuaji endelevu wa sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad