Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameiomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kusimamia kikamilifu utoaji wa hati za ardhi ili kuhakikisha zinazingatia taratibu na mipango miji, akisema kuwa uzembe katika mchakato huo unachangia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi.
“Tusipofuata taratibu za upangaji miji, tutazalisha migogoro mikubwa katika jamii. Watu wanajikuta wanaziba barabara au kujenga katika hifadhi za wazi kwa sababu ya makosa ya kiutendaji,” alisema Mpogolo.
Aidha, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Samia Ardhi Kliniki ili kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara ya Ardhi, ikiwemo ushauri wa kitaalamu, uhakiki wa nyaraka, pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Katika hatua nyingine, Mpogolo ameipongeza Wizara ya Ardhi kwa kuanzisha kliniki hiyo, akieleza kuwa itasaidia kupunguza malalamiko ya muda mrefu na kuimarisha uwazi pamoja na uwajibikaji katika sekta ya ardhi.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha mipango miji inaheshimiwa na maendeleo yanafanyika kwa utaratibu unaokubalika kisheria.

No comments:
Post a Comment