

Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, ameagiza kuimarishwa kwa udhibiti wa taaluma ya uandishi wa habari nchini ili kulinda hadhi ya tasnia hiyo na kuongeza imani ya umma kwa vyombo vya habari.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 4, 2026, wakati wa ziara yake katika Ofisi za Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Naibu Waziri huyo alisisitiza kuwa ni wakati wa bodi hiyo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari kwa kuhakikisha wanaojihusisha na kazi za habari wanakuwa na ithibati halali.


Alieleza kuwa kukithiri kwa watu kufanya kazi za habari bila usajili rasmi kunachangia kushuka kwa viwango vya taaluma na kuathiri taswira ya sekta hiyo, hivyo akaitaka JAB kuongeza kasi ya usajili, utoaji wa vitambulisho vya uandishi (Press Cards) na ufuatiliaji wa mienendo ya vyombo vya habari hususan vya mtandaoni.
“Ni lazima kulinda heshima ya taaluma hii. Uandishi wa habari ni mhimili muhimu katika ujenzi wa taifa, hivyo usimamizi wake haupaswi kulegalega,” alisisitiza.
Katika taarifa yake kwa Naibu Waziri, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo, hatua kubwa zimepigwa ikiwemo uanzishaji wa mifumo ya kidijitali ya usajili wa waandishi, utoaji wa ithibati na vitambulisho rasmi, pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu maadili ya taaluma.
Hata hivyo, alibainisha kuwa bodi hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo uhitaji wa rasilimali zaidi na changamoto za udhibiti wa maudhui katika vyombo vya habari vya mtandaoni ambavyo vinaongezeka kwa kasi.
Ziara hiyo imekuja katika kipindi ambacho sekta ya habari nchini inaendelea kukua sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano, hali inayodai uwajibikaji mkubwa zaidi kwa wadau wote ili kuhakikisha taaluma ya uandishi wa habari inabaki kuwa chombo cha kuhabarisha kwa weledi, maadili na uwajibikaji



No comments:
Post a Comment