Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Dkt.Zabron Masatu akizungumza na maafisa wa TASAC waliotembelea Ofisi ya Mkoa wa Mara.
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Mkoa wa Mara imewataka Wavuvi na wamiliki wa vyombo vidogo vya majini kulazimisha safari za majini pindi wanapoona viashiria vya hatari ya hali ya hewa katika kipindi hiki cha mvua.
Hayo ameyasema Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron Masatu wakati akizungumza na maafisa wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) walioko katika zoezi la kutoa elimu ya usalama majini.
Dkt.Masatu amesema kuwa ni wajibu wa kila mmiliki, mvuvi na wasafirishaji kuhakikisha usalama wa maisha unatangulizwa mbele ya tamaa ya kipato. Ameeleza kuwa mara nyingi ajali hutokea kwa sababu ya kupuuza viashiria vya hatari, ikiwemo taarifa za hali ya hewa ikiwemo mawimbi makali, mvua kubwa na upepo mkali unaoambatana na msimu huu mvua za masika.
“Ni bora kuchelewesha safari kuliko kupoteza maisha,” amesisitiza.
Kwa upande wao, Afisa Mfawidhi wa Mkoa wa Mara, Hezron Lusangija pamoja Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Rorya, Godfrey Bwatondi, wameendelea kutoa elimu kwa wavuvi na wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vifaa okozi, hususan maboya (life jackets), wakieleza kuwa vifaa hivyo si mzigo bali ni kinga ya uhai wawapo kwenye shughuli mbalimbali za kusafiri au kuvua. Wamesema kuwa kumekuwa na dhana potofu miongoni mwa baadhi ya wavuvi kwamba kuvaa jaketi okozi kunawapa usumbufu, jambo ambalo ni linahatarisha maisha yao mara ajali inapotokea kwa vyombo vidogo.
TASAC imeeleza kuwa kampeni ya elimu ya usalama majini inalenga kuwakumbusha wadau wote kufuata Sheria na taratibu zilizowekwa, ikiwemo kuhakikisha kila chombo kinachoingia majini kinakuwa na maboya yenye idadi inayolingana na abiria. Elimu hiyo pia inalenga kuondoa tabia ya wavuvi na wananchi kuvaa maboya vibaya au kuvua mara wanapofika majini, wakijiamini kuwa uwezo wa kuogelea unatosha au watavaa mara ajali itakapotokea, kitu ambacho hakiwezekani pale inapotokea.
Wananchi wa Rorya na maeneo jirani wamepongeza juhudi hizi, wakisema elimu inayotolewa imekuwa msaada mkubwa katika kuimarisha usalama na kupunguza ajali. Wamesema kuwa kampeni hii imewasaidia kuelewa kuwa jaketi okozi ni ngao ya uhai na si mzigo wa gharama.
Serikali ya Mkoa wa Mara imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo TASAC ili kuhakikisha usalama wa wananchi unakuwa kipaumbele, na kwamba hakuna maisha yanayopaswa kupotea kwa sababu ya uzembe au kupuuza tahadhari za hali ya hewa


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment