Na Mwandishi wa OMH Arusha.
MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ametoa wito kwa wakurugenzi wa bodi na watendaji wakuu wa kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache kuachana na usimamizi wa kawaida na kuelekea kwenye uongozi wa kimkakati unaotazama mbele.
Wito huo umetolewa wakati wa Mkutano wa Wakurugenzi wa Kampuni ambazo Serikali ina hisa hisa chache (MIF 2026) unaofanyika kwa siku tatu jijini Arusha, kuanzia Jumatatu, Machi 16, 2026.
Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Mchechu alisema mabadiliko haya ni muhimu ili kampuni ziweze kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia, sambamba na kutumia kikamilifu fursa zinazojitokeza.
Alisisitiza kuwa taasisi zitakazojenga utamaduni wa ubunifu, fikra za mbele na maamuzi ya haraka ndizo zitakazofanikiwa zaidi na kuchangia kwa ufanisi katika kufikia malengo ya Dira 2050.
Bw. Mchechu alisema jukwaa hilo, ambalo linafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024, limekuwa sehemu muhimu kwa viongozi wa kampuni kujadili masuala ya utawala bora, utendaji na mchango wao katika mageuzi ya uchumi wa Tanzania.
Aliongeza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu, “Kutoka Ufuatiliaji wa kawaida hadi Uongozi wa Kimkakati unaotazama mbele,” inaakisi umuhimu wa bodi na viongozi wakuu kuacha usimamizi wa kawaida na badala yake kuendeleza uongozi unaoweza kutambua mapema changamoto na fursa za baadaye.
“Katika dunia ya leo inayobadilika kwa kasi kiuchumi na kiteknolojia, uongozi hauwezi tena kujikita tu kusimamia hali ya sasa, bali unapaswa kutazama mbele na kujiandaa kwa siku za usoni,” alisema.
Alisisitiza kuwa taasisi zinazojenga utamaduni wa kufikiri mbele, ubunifu na maamuzi ya haraka ndizo zitakazofanikiwa zaidi na kuchangia kwa ufanisi katika kufikia malengo ya Dira 2050.
Bw. Mchechu pia alieleza kuwa uwekezaji wa Serikali katika kampuni zenye hisa chache umeongezeka kutoka Sh821 bilioni hadi Sh3.6 trilioni, huku michango ya gawio ikipanda kutoka Sh58 bilioni hadi Sh266 bilioni, ongezeko la asilimia 357 katika kipindi cha miaka mitano.
Mkutano wa MIF 2026 umewakutanisha zaidi ya washiriki 200, wakiwemo wakurugenzi wa bodi, Maafisa wakuu, watunga sera na wataalamu kutoka ndani na nje ya Tanzania kujadili mikakati ya kuimarisha utendaji na utawala wa kampuni hizo, ili ziweze kuchangia kwa ufanisi katika maendeleo ya uchumi wa taifa.


No comments:
Post a Comment