📍Sababu kubwa yaelezwa kushindwa kuiondoa baa ya Thinkers
📍Mwenyekiti Ustadh Rajab ashusha maelekezo mazito
Na Mashaka Mhando, Tanga
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, imemuagiza Katibu wa CCM Mkoa kusitisha mkataba wa Meneja wa Uwanja wa Mkwakwani, Akida Machai, kufuatia kusuasua kwa utendaji na usimamizi mbovu wa miundombinu ya uwanja huo wa kihistoria.
Maamuzi hayo magumu yamefikiwa Leo Machi 11 2026 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Komredi Rajab Abdurahman, wakati wa ziara maalum ya Kamati ya Siasa ya Mkoa iliyolenga kukagua maendeleo ya ukarabati na hali ya uwanja huo unaomilikiwa na Chama.
Akizungumza kwa uchungu mbele ya wajumbe wa kamati hiyo, Mwenyekiti Rajab alisema Chama hakiwezi kuvumilia uzembe wa mtendaji mmoja unahatarisha hadhi ya uwanja huo, huku CCM ikigharamia mahitaji yote muhimu ikiwemo maji na umeme bila kupata tija inayostahili.
“CCM tunatoa fedha kuhakikisha wananchi wanapata burudani, lakini usimamizi ni sifuri. Mimi binafsi nilitafuta milioni 50 kutoka kwa wadau kwa ajili ya maboresho, sasa kwa sababu yeye (Meneja) hajui uchungu wa kutafuta fedha hizo, ameuacha uwanja unakuwa kama mbuga ya wanyama. Hili halikubaliki,” alisema Mwenyekiti Rajab.
Mwenyekiti alieleza kushtushwa na kitendo cha viti vya uwanja kukaa muda mrefu bila kufungwa mpaka vimeanza kuota majani, hali inayoweza kuupelekea uwanja huo kufungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).
Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti Rajab ametoa maelekezo kwa Kamati ya Siasa Mkoa kukaa haraka na kuteua Meneja mwingine mwenye uwezo na uchungu wa mali za Chama, atakayehakikisha viti hivyo vinafungwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.
Mbali na kumuondoa Meneja, Mwenyekiti pia ameamuru kuondolewa mara moja kwa mpangaji wa baa iliyopo nje ya uwanja huo, ambayo imetajwa na TFF kuwa ni kizuizi kwa usalama na uingiaji wa washabiki uwanjani.
“Huyu mpangaji ana mapembe kiasi gani mpaka agomee maelekezo ya Chama na TFF? Nahitaji hii baa iondoke leo ili maagizo ya mamlaka za soka yatimizwe. Lazima apatikane Meneja atakayeshirikiana nasi kurudisha heshima ya Mkwakwani,” alisisitiza Komredi Rajab.
Kwa upande wake, aliyekuwa Meneja wa uwanja huo, Akida Machai, ameshukuru CCM kwa fursa aliyopewa na kudai kuwa changamoto ya nguvu kazi ndiyo iliyokwamisha ufungaji wa viti hivyo, huku akibainisha kuwa alishawasilisha bajeti ya kazi hiyo kwa uongozi wa Chama.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
No comments:
Post a Comment