MWANZA, Machi 28, 2026.
KUNDI la wafanyakazi wanawake wa Airtel Tanzania mkoani Mwanza siku ya Jumamosi walitembelea kituo cha watoto yatima kilichopo Busweru na kutoa msaada wa chakula, mavazi na mahitaji mengine muhimu ikiwa ni sehemu ya mpango wa kampuni wa kushirikiana na jamii.
Kundi hilo linalojulikana kama Airtel Divas Mwanza lilitoa mahitaji ya msingi ikiwemo vyakula, bidhaa za usafi na mavazi kwa watoto wanaoishi katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Watoto wa Afrika, katika mpango ambao kampuni imesema unaakisi dhamira yake pana ya kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii.
Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za uwajibikaji kwa jamii za Airtel Tanzania, zinazolenga maendeleo ya jamii pamoja na programu zinazowawezesha wanawake na kusaidia watoto na makundi mengine yenye uhitaji.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Jackline Kaaya, Meneja wa Maduka wa Airtel Kanda ya Ziwa wa Airtel Mwanza na mwakilishi wa Airtel Divas, alisema mpango huo unalenga kuwasaidia watoto huku ukiimarisha uhusiano wa kampuni na jamii inayozunguka.
“Katika Airtel, tunaamini mafanikio ya taasisi yoyote yanahusiana moja kwa moja na ustawi wa jamii inayozunguka. Kupitia Airtel Divas, tunaendelea kusaidia wanawake, watoto na makundi mengine yenye uhitaji, si tu kwa kutoa misaada bali pia kwa kuonesha mshikamano na kujali,” alisema Kaaya.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Makao ya Kulelea Watoto Wenye Mahitaji Maalum ya Mtoto wa Afrika, Bw. Peter Onyango, pamoja na baadhi ya watoto wanaolelewa katika makao hayo, wameishukuru kampuni ya Airtel kwa msaada huo huku wakitoa wito kwa taasisi na makampuni mengine kuiga mfano huo kwa kuvisaidia vituo vinavyolea watoto wenye mahitaji maalum.
“Niwashukuru sana Airtel kwa moyo wao wa kujitolea na msaada huu muhimu. Tunatoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huu ili kusaidia kuboresha maisha ya watoto wenye mahitaji maalum,” alisema Peter Onyango, Afisa Ustawi wa Makao ya Mtoto wa Afrika.
Naye Vaileth Ramadhan, mmoja wa watoto wanaolelewa katika makao hayo, alisema msaada huo umewaletea faraja kubwa.
“Tunaishukuru Airtel kwa kutukumbuka na kutuletea mahitaji haya muhimu. Hii imetufanya tujisikie kuthaminiwa na kupendwa,” alisema Vaileth Ramadhan.
Mbali na kukabidhi msaada huo, wafanyakazi hao walitumia muda kushirikiana na watoto kupitia michezo na shughuli za kijamii zilizolenga kuwapa faraja na msaada wa kihisia.
Airtel Tanzania imesema kuwa mpango wa Airtel Divas unawaleta pamoja wafanyakazi wanawake kutoka maeneo mbalimbali kushiriki katika programu za kijamii zinazochangia ustawi wa jamii na kuhamasisha ushirikishwaji.
Katika miaka ya hivi karibuni, kampuni imekuwa ikiunga mkono miradi mbalimbali ya kijamii nchini Tanzania, hususan ile inayolenga elimu, afya na kusaidia makundi yenye uhitaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake mpana wa uwajibikaji kwa jamii.

.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)

No comments:
Post a Comment