HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 25, 2026

World Vision Tanzania Yaimarisha Programu za Ulinzi wa Watoto

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo katika kuboresha ustawi wa jamii na watoto nchini. 

Akizungumza leo Februari 25, 2026 katika uzinduzi wa mkakati wa miaka Mitano wa World Vision Tanzania uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Waziri Gwajima alisema kuwa jitihada za pamoja zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwafikia watoto na familia nyingi zilizo katika mazingira magumu.

Alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuboresha malezi, elimu, afya na ulinzi wa watoto. 

Aidha, aliipongeza World Vision Tanzania kwa kazi kubwa wanayofanya katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo kuwajengea uwezo wanawake na vijana kiuchumi, kuimarisha ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili, pamoja na kusaidia jamii kupata maji safi na huduma muhimu za kijamii.

Waziri Gwajima pia alibainisha kuwa mkakati mpya wa shirika hilo unalenga kuwafikia mamilioni ya watoto na kuimarisha mifumo ya kijamii inayosaidia ustawi wa jamii.

 Alisema serikali itaendelea kushirikiana na mashirika ya maendeleo ili kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Katika hotuba yake, alitoa wito kwa wadau wote, ikiwemo sekta binafsi, viongozi wa dini na wananchi, kuendelea kushiriki katika programu zinazolenga maendeleo ya watoto na familia. 

Alisisitiza kuwa uwekezaji katika ustawi wa watoto ni msingi muhimu wa kujenga rasilimali watu bora kwa maendeleo ya taifa.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya World Vision Tanzania, Victori Elangwa, alisema mkakati huo umejengwa juu ya imani kwamba mabadiliko ya kweli hutokea pale wadau wanapotembea pamoja kwa mshikamano na uwajibikaji wa pamoja. 

Aidha, Elangwa alieleza kuwa taasisi hiyo inaadhimisha utekelezaji wa mpango wa WASH unaoweka kipaumbele kwenye maji safi, usafi wa mazingira na nishati, akibainisha kuwa huduma hizo ni msingi wa afya bora na mafanikio ya kielimu kwa watoto. 

Alisema watoto wanapopata maji safi ya kunywa, shule na vituo vya afya vinapokuwa na mifumo bora ya maji na usafi, pamoja na jamii kujengewa uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, matokeo yake huwa ni mabadiliko chanya yanayoonekana katika maisha yao.

Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na uongozi wake madhubuti, pamoja na wadau na marafiki mbalimbali wanaoamini katika uwezo wa kila mtoto. 

Elangwa alitoa wito kwa wananchi, taasisi za binafsi, mashirika na jumuiya kushiriki kikamilifu katika harakati hizo kwa kuchangia, kushirikiana na kuunga mkono dhamira ya kuhakikisha hakuna mtoto anayesalia nyuma katika safari ya maendeleo ya taifa.






































No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad