JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 45 na gramu 785, zilizokuwa zikisafirishwa kwa mabasi ya abiria kuelekea Dar es Salaam.
Watuhumiwa hao ni Wilfred Komba (24), mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Iringa, Lenad Shamba maarufu Paulo (21), mkazi wa Tarime mkoani Mara, James Mwakalebela (26), mkazi wa Ngonga – Kyela na Joseph Mkwara maarufu Aliki (26), mkazi wa Kyela.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, watuhumiwa hao walikamatwa katika nyakati tofauti wakiwa na dawa hizo za kulevya zilizofichwa kwenye mabegi matatu na mifuko miwili ya sandarusi. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa bangi hizo ziliingizwa nchini kutoka nchi jirani.
NDUGU WA FAMILIA MOJA WASHIKILIWA KWA MAUAJI YA MZEE MWENYE MIAKA 87
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia ndugu wa familia moja kwa tuhuma za kumuua mzee mwenye umri wa miaka 87, Jenti Segelela, mkazi wa Busoka – Masebe.
Watuhumiwa ni Solomon Mwambyale (68) pamoja na watoto wake wawili, Stephano Mwaisango (32) na Emmanuel Mwaisango (36). Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa shemeji wa mtuhumiwa Solomon Mwambyale.
Tukio hilo lilitokea Februari 7, 2026 katika Kitongoji cha Busoka, Kijiji cha Lusungo, Kata ya Makwale, ambapo watuhumiwa walimdaiwa kumkata marehemu kwa kitu chenye ncha kali kisogoni na kisha kutoroka.
Baada ya tukio hilo, Polisi walianzisha msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote watatu Februari 8, 2026 saa 7 usiku. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa mashamba ya ukoo pamoja na tamaa ya kujipatia mali kwa njia isiyo halali.
WAWILI WASHIKILIWA KWA KUINGILIA MIFUMO YA MAKAMPUNI YA UKOPESHAJI SIMU
Aidha, Polisi Mkoa wa Mbeya wanawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuingilia mifumo ya kibiashara ya makampuni ya kukopesha simu.
Watuhumiwa ni Charles Oden maarufu Mwakasege (32), fundi simu na mkazi wa Meta pamoja na Isack Charles maarufu Bebwa, mkazi wa Shewa, jijini Mbeya.
Watuhumiwa walikamatwa katika misako iliyofanyika kati ya Januari 27 na Februari 5, 2026 katika eneo la Rungwe Music, Mwanjelwa. Inadaiwa wamekuwa wakibadili simu zilizokopwa na kuondoa mifumo ya ufuatiliaji ili wateja wasiweze kufuatiliwa na makampuni husika.
Katika upekuzi uliofanyika kwenye ofisi zao, Polisi walikamata simu mbalimbali zikiwemo Samsung A53, Infinix 21, Tecno 13, Itel 11 na Yas 1 pamoja na vifaa vya kuflashia simu na laptop tatu. Ukaguzi wa awali umebaini baadhi ya simu hizo ni mali ya makampuni ya ukopeshaji na nyingine ziliripotiwa kuibwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa wito kwa wananchi kuacha mara moja kujihusisha na uingizaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, likisisitiza kuwa ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya na mustakabali wa jamii, hususan vijana. Pia limewahimiza wananchi kuacha tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali na badala yake kujishughulisha na shughuli halali, likisisitiza kuwa uhalifu haulipi.
Imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.

No comments:
Post a Comment