HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 10, 2026

WANAFUNZI WA MUM WATINGA NBAA KUPATA ELIMU YA UHASIBU


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kutoa elimu/mafunzo kwa Vyuo vikuu pamoja na Shule za Sekondari ikiwa na lengo la kuwajengea ufahamu kuhusu shughuli mbalimbali za Bodi na kukuza taaluma ya Uhasibu.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Huduma za Shirika kutoka NBAA CPA Kulwa Malendeja kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA CPA Pius Maneno amekipongeza chuo hicho kwa kuwa na mwendelezo wa kuwaleta wanachuo wanaosoma masomo ya Uhasibu na Biashara kwenye Bodi hiyo ili kupata elimu kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Bodi.

Malendeja amesema ili kuwa Mhasibu au Mkaguzi inabidi kufanya mitihani ya Bodi hiyo ili kupewa cheti cha kitaaluma ili uweze kutambulika kisheria kama Mhasibu au Mkaguzi ambapo cheti hicho kitakutambulisha kitaifa na kimataifa na kuweza kufanya kazi nje na ndani ya nchi.

"Nimefarijika kuona wanafunzi wa Sheria pia  wakishiriki katika ziara hii na kupata mafunzo kwani wana nafasi ya kusomea masomo ya Uhasibu na kuwa CPA yaani "Certified Public Accountant" alisema Malendeja

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya amesema ziara hiyo imekuwa chachu kwa wanafunzi kwani wanapata taarifa mbalimbali kuhusu NBAA

Aliongeza kuwa kupitia matukio  mbalimbali NBAA husikiliza maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu huduma zake kwa mfano NBAA imesikia kilio cha wadau wake kuhusu ucheleweshwaji wa vyeti vya Kitaaluma kwa kuomba Bodi kusaidia upatikanaji wa vyeti mapema wanapomaliza na sio kwa kusubiri kwa muda mrefu. Na sasa NBAA imeamua kuanzisha Mahafali nyingine ili kukidhi mahitaji ya wadau wake, na kwa mara ya kwanza mahafali hayo yatafanyika tarehe 28 Machi, 2026 katika ukumbi wa APC Bunju jijini Dar es Salaam. Maana yake kwa mwaka kutakuwa na mahafali mbili yaani Machi na Septemba au Oktoba mwanzoni.

Naye mwalimu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro Dkt. Ayubu Timba ameishukuru NBAA kwa mwaliko wa wanafunzi kuja kupata Elimu ya Uhasibu.

Aliongeza kuwa wanachuo hao waliotembelea na kupata elimu ya Uhasibu itawapa dira na mwelekeo mzuri sasa na hapo baadae na pia aliwasisitiza wanachuo hao kwenda kuwa mabalozi kwa wenzao na jamii kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Huduma za Shirika kutoka NBAA CPA Kulwa Malendeja akitoa salamu za Bodi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA Pius A. Maneno wakati wa ziara ya masomo ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro waliotembelea Bodi hiyo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ya Bodi.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya akitoa mada kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na NBAA "NBAA Overview"  kwa wanachuo wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro waliotembelea Bodi hiyo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ya Bodi.
CPA Esther Masalla akiwasilisha mada kuhusu uanachama, jinsi ya kupanda daraja na usajili wa makampuni ya kihasibu na kikaguzi wakati wa ziara ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro.
CPA Praygod Munuo akitoa mada kuhusu misingi ya fedha kwa wanachuo wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro
Rebecca Siame akizungumzia usajili, madaraja mbalimbali ya mitihani ya Taaluma ya Uhasibu na jinsi ya kufanya mitihani hiyo kwa wanachuo wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro
Rais wa  wanafunzi wanaosoma masomo ya Uhasibu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUMASO)  Benjamin Mussa akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa NBAA kufuatia kufanikishwa kwa ziara yao katika ofisi hiyo
Baadhi ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro wakichangia mada pamoja na kuuliza maswali kwa watoa mada mbalimbali wakati wa ziara yao ofisi za NBAA jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanachuo wanaosoma masomo ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinatolewa na wataalamu kutoka NBAA.
Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro Dkt. Ayubu Timba akitoa neno la shukrani kwa NBAA kwa niaba ya uongozi wa chuo hicho.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro wanaosoma masomo ya Uhasibu mara baada ya kumaliza mafunzo yaliyofanyika katika ofisi za Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad